Upelelezi kesi ya Meneja wa Tume ya Madini, mbioni kukamilika

Wednesday August 7 2019

By Hadija Jumanne,Mwananchi [email protected]

Dar Es Salaam. Upelelezi katika kesi ya wizi wa madini ya dhahabu yenye thamani ya Sh507 milioni, inayomkabili Meneja wa Maabara  Tume ya Madini, Donald Njonjo (30) na wenzake wawili, upo katika hatua za mwisho kukamilika.

Njonjo na wenzake wanakabiliwa na mashtaka manne ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam nchini Tanzania.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon ameieleza Mahakama hiyo, leo Jumatano Agosti 7, 2019, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Simon amedai  mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Kelvin Mhina, kuwa upelelezi wa shauri hilo upo katika hatua za mwisho kukamilika, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Mhina baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka ameahirisha kesi hiyo hadi, Agosti 21, 2019 kesi hiyo itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutoka na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.

Mbali na Njonjo, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Gamba Muyemba (51) maarufu Emmanuel ambaye ni mkazi wa Tandika na Kashif Mohamed (41) mkazi wa Upanga, ambao kwa pamoja wanadaiwa kuiba madini hayo kwenye Tume ya Madini.

Advertisement

Washtakiwa hao walifikishwa Kisutu kwa mara ya kwanza, Julai 15, 2019 wakikabiliwa na mashtaka hayo.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Novemba 30, 2017 na Juni 29, 2019 katika Ofisi ya Tume ya Madini iliyopo Masaki wilayani Kinondoni.

Inadaiwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa hao waliiba mdini ya dhahabu yenye uzito wa Kilogramu 6.244 yenye thamani ya Sh507.3 milioni  mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika shtaka la pili, Julai 8, 2019 katika maeneo ya Mtaa wa Indiragandhi wilayani Ilala, Mohamed alikutwa na madini ya dhahabu yenye uzito wa gramu 2794.5 yakiwa na thamani ya Dola za Marekani 121,155.45 sawa na Sh 278,714,478.06 yaliyoibwa Tume ya Madini.

Vilevile, kati ya Julai Mosi, 2018 na  Novemba 31, 2018, katika maeneo mbalimbali ya wilayani Ilala, washitakiwa kwa pamoja waliuza madini ya dhahabu yenye uzito wa Kilogramu 6.244 yenye thamani ya Sh507.3 milioni bila kupata kibali.

Katika shtaka la nne, kati ya Julai Mosi, 2018 na Novemba 31, 2018 katika maeneo mbalimbali, washtakiwa hao walijihusisha moja kwa moja na muamala unaohusu madini wakati wakijua fedha hizo zinatokana na makosa ya wizi.

Advertisement