Upelelezi wa ndani, kesi ya kigogo wa Takukuru wakamilika, Hakimu atoa agizo

Muktasari:

  • Upelelezi wa ndani katika kesi uhujumu uchumi inayomkabili, aliyekuwa Mkurugenzi  wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathimini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru), Kulthum Mansoor, umekamilika na sasa upande wa mashtaka unasubiri taarifa kutoka nchi nje ya nchi.

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili, aliyekuwa Mkurugenzi  wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathimini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Tanzania, Kulthum Mansoor umesema unasubiri taarifa na vielelezo kutoka nje ya Tanzania.

Ni baada ya upelelezi wa ndani ya nchi kukamilika.

Mansoor anakabiliwa na mashtaka nane, likiwamo la utakatishaji fedha kiasi cha Sh1.4bilioni, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon ameieleza mahakama hiyo, leo Jumatatu Januari 20, 2020 wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Simon amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Godfrey Isaya, kuwa upelelezi wa ndani wa kesi hiyo umeshakamilika na sasa wanasubiri taarifa kutoka nchi mbili, ambazo hakuwa tayari kuzitaja.

“Upelelezi upo katika hatua nzuri na niseme tu upelelezi wa ndani umeshakamilika na kinachosubiriwa kwa sasa ni upelelezi kutoka katika nchi mbili ambazo hatuwezi kuzitaja kwa sasa,” amedai Simon

“Kutokana na hali hii, tunaiomba mahakama yako ipange tarehe nyingine kwa ajili kutajwa,” amedia.

Simon baada ya kueleza hayo, Elia Mwingira ambaye ni wakili wa Kuluthum, aliomba upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi huo kwa wakati ili kesi iweze kuendelea na hatua nyingine.

Hakimu Isaya baada ya kusikiliza hoja za pande zote aliutaka upande wa mashtaka kuhakikisha wanafuatilia taarifa katika nchi hizo ili kesi hiyo iweze kuendelea mbele.

Isaya baada ya kueleza hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 3, 2020 kesi hiyo itakapotajwa.

Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili kuwa halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

 

Katika kesi ya msingi, Kwa mujibu ya hati ya mashtaka inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari, 2013 na Mei 2018, mshitakiwa alighushi barua ya ofa ya Agosti 13,  mwaka 2003 kwa madhumuni ya kuonyesha kuwa, barua hiyo imetolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo huku akijua kuwa sio kweli.

 

Katika mashitaka ya pili, inadaiwa kati ya Januari,2012 na Mei 2017, Upanga Wilaya ya Ilala, mshitakiwa kwa kudanganya alijipatia Sh 5.2.milioni , kutoka kwa Alex Mavika ambaye ni mfanyakazi wa Takukuru kama malipo ya kiwanja kilichopo Kijiji cha Ukuni Bagamoyo.

 

Pia inadaiwa kati ya tarehe hizo, Mansoor alijipatia Sh3 milioni kutoka kwa Wakati Katondo kama malipo ya kiwanja kilichopo maeneo ya Kijiji cha Ukuni wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

 

Katika mashtaka ya utakatishaji fedha, inadaiwa kati ya Januari mwaka  2013 na Mei mwaka jana huko maeneo ya Upanga, mshitakiwa alijipatia sh.1,477,243,000 wakati akijua kuwa fedha hizo ni haramu na ni zao la kosa tangulizi la kughushi.