Upelelezi wakwamisha kesi ya kigogo wa Takukuru

Wednesday September 18 2019

By Fortune Francis, Mwananchi [email protected]

Dar es salaam. Kesi inayomkabili  aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathimini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Kulthum Mansoor (57) inahitaji msaada wa kisheria kutoka nje ya Tanzania kwa ajili ya kusaidia upelelezi.

Mansoor anakabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi ikiwamo manane ya kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha Sh1.477 bilioni.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Saimon amedai leo Jumatano Septemba 18,2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Kevini Mhina kuwa kuna maombi ya msaada wa kisheria kutoka nje ya nchi yanayosubiriwa.

"Kesi imekuja kwaajili ya kutajwa upelelezi haujakamilika kutokana na maswala mengi ya kisheria ikiwemo kuomba msaada kutoka nje ya nchi tunaousubiri," amedai wakili Wankyo

Hakimu Mhina baada ya maelezo hayo ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 2, 2019 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayomkabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kati ya Januari 2013 na Mei, 2018 ofisi za Takukuru zilizopo Upanga jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alighushi barua ya ofa ya Agosti 13, 2003 kwa madhumuni ya kuonyesha barua hiyo imetolewa na Halmashauri ya wilaya  Bagamoyo huku akijua kuwa siyo kweli

Advertisement

 

Shtaka la pili, ilidaiwa kati ya Januari 2012 na Mei, 2017 eneo la Upanga Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathimini Takukuru, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh5.2 milioni kutoka kwa Alex Mavika.

 

Ilidaiwa mshtakiwa alijipatia fedha hizo baada ya kudanganya kwamba angemuuzia kiwanja kijiji cha Ukuni Wilaya ya Bagamoyo, Mkoani Pwani.

 

Katika shtaka la tatu hadi la saba tarehe na mahali pa tukio la pili, mshtakiwa alijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu Sh27 milioni kutoka kwa watu watano tofauti.

 

Wankyo alidai mshtakiwa alijipatia fedha kutoka kwa Wakati Katondo, Sh3 milioni, Gogo James, Sh5 milioni, Ekwabi Majungu, Sh7 milioni, John Amos Sh7 milioni na Rose Anatory Sh5 milioni  wote wanadaiwa kuwa watumishi wa Takukuru.

Katika shtaka la nane,  kati ya Januari, 2013 na Mei, 2018 eneo la Upanga, jijini Dar es Salaam mshtakiwa alitakatisha Sh1,47 milioni  wakati akijua kuwa  fedha hizo ni zao  la kosa tangulizi la kughushi.

 

Advertisement