VIDEO: Upinzani wataka nafasi zaidi ya kuchangia bungeni

Mnadhimu wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani Bungeni, Ester Bulaya akiomba muongozo wakati wa kikao cha sita cha mkutano wa 18 wa Bunge, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nchini Tanzania imeomba Bunge kuongeza idadi ya wabunge watakaochangia  taarifa za kamati za chombo hicho cha Dola zilizowasilishwa bungeni leo Jumanne Februari 4, 2020.

Dodoma. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nchini Tanzania imeomba Bunge kuongeza idadi ya wabunge watakaochangia  taarifa za kamati za chombo hicho cha Dola zilizowasilishwa bungeni leo Jumanne Februari 4, 2020.

Leo wabunge wanajadili taarifa za utekelezaji wa shughuli za kamati tatu za utawala na Serikali za mitaa, katiba na sheria pamoja na sheria ndogo.

Akiomba mwongozo wa Spika bungeni leo mnadhimu wa Kambi Rasmi ya upinzani bungeni, Ester Bulaya amesema hawawezi kuwanyima wabunge hasa wa upinzani kutoa maoni yao kwa kamati muhimu kwa sababu ya kisingizio cha muda.

 “Kwa mujibu wa kanuni zetu za Bunge kiti chako kinaweza kuongeza muda hadi pale shughuli zitakapokamilika. Mwenyekiti hatuwezi kuwanyima wabunge hasa Kambi Rasmi ya Bungeni  kutoa maoni yao katika kamati muhimu za leo,” amesema.

Amesema wanaomba wapewe nafasi za nyongeza za kuchangia ili wabunge wapate nafasi za kutoa maoni yao.

“Tunajadili kamati mbili upande wa Chadema tunapata, CUF wanapata nafasi ya ziada, leo tunajadili kamati tatu mnatoa CUF nafasi moja na Chadema nafasi mbili,” amesema.

Ameomba haki itendeke kwa vyama hivyo katika nafasi za uchangiaji.

Akijibu suala hilo mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga amesema ratiba za Bunge zinaenda kwa mujibu wa utaratibu na kwamba ratiba yao ya leo nafasi za Chadema ni mbili na CUF ni moja.

“Kwa hiyo kama mnataka kuchangia zaidi mgawane dakika kazi itakwenda,” amesema Najma na kuruhusu kuendelea na shughuli zilizopangwa.