Ushauri wa Ndugai kuhusu biashara mazao ya kilimo

Muktasari:

  • Spika Job Ndugai ametoa ushauri huo jana Jumatano Aprili 17,2019 katika mhadhara kwa umma kuhusu mwelekeo wa upatikanaji chakula na kukuza mnyororo wa thamani wa bidhaa zitokanazo na kilimo duniani.

Dodoma. Spika Job Ndugai ameishauri Serikali mambo manne ya kufanya kwa ajili ya maendeleo ya biashara zitokanazo na mazao ya kilimo na viwanda vya usindikaji   nchini.

Ndugai ametoa ushauri huo jana jioni Jumatano Aprili 17, 2019 katika ukumbi wa Msekwa uliopo bungeni jijini Dodoma katika mhadhara kwa umma kuhusu mwelekeo wa upatikanaji chakula na kukuza mnyororo wa thamani wa bidhaa zitokanazo na kilimo duniani.

Katika mhadhara huo ulioandaliwa na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Groningen cha Uholanzi, Profesa  Jan Willem Velthuizen wa chuo hicho alizungumzia hali ya chakula duniani na kushauri uzalishaji lazima uongezeke kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu.

“Kwanza, Serikali lazima iendelee kuweka mazingira mazuri ya sera ambazo zitawafanya wafanyabiashara wadogo na wa kati wa viwanda vinavyosindika mazao ya kilimo kukua na kustawi,” amesema Ndugai.

Amesema jambo la pili ni wazalishaji wadogo kupatiwa msaada wa kuwawezesha kushindana katika soko la ndani, kikanda na kimataifa.

“Kwa mfano mafunzo yanaweza kusaidia kuboresha stadi zao za usimamizi mzuri wa shughuli zao. Hili IFM mnaweza kusaidia kutoa elimu na stadi za biashara katika kilimo,” amesema.

Ndugai amesema jambo la tatu ni upatikanaji dhaifu wa huduma za fedha kwa muda mrefu kwamba zimedumaza maendeleo vijijini nchini na kushauri mambo hayo kushughulikiwa kwa ujumla wake.

“Natambua kuwa upatikanaji huduma za fedha umeboreshwa kutokana na maendeleo ya ukopeshaji wa fedha vijijini,” amesema Ndugai.

Amesema jambo jingine ni uwekezaji katika utafiti wa kilimo, kwamba ni muhimu ili kuibua teknolojia mpya  ambazo zinaweza kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Uwekezaji katika tafiti mara nyingi hutoa matokeo mazuri. Ili kuweza kupata mafanikio katika haya yaliyopendekezwa kuna haja ya kuongeza uwekezaji wa umma katika sekta ya kilimo,” amesema Ndugai.

Amesema rasilimali fedha za kutosha zinapaswa kuelekezwa katika tafiti za kilimo ili kuhakikisha wakulima wadogo wanaweza kukabiliana na tabianchi kwa kutumia mbegu bora zinazohimili ukame.

“Fedha za umma zinapaswa kuelekezwa katika miradi ya umwagiliaji, kujenga maghala ya kuhifadhi mazao, kuhakikisha upatikanaji pembejeo za kilimo na kuendeleza uwiano wa uzalishaji na masoko,” amesisitiza Ndugai.

Naye Profesa Velthuizen amesema idadi ya watu inaongezeka duniani lakini haiendani na uzalishaji wa chakula.

“(Mwaka) 2030 idadi ya watu itakuwa bilioni 8.5, je tunaendeleaje huko. Tutahitaji asilimia 60 zaidi ya umeme; asilimia 40 zaidi ya maji na asilimia 35 zaidi ya chakula,” amesema.