IMANI POTOFU: Ushirikina watanda mauaji ya mwanafunzi - VIDEO

Ndugu wa Mwanafunzi wa darasa la Pili aliyekuwa anasoma Shule ya Msingi Jitihada iliyopo Halmashauri ya Mji wa Kibaha Mkoa wa Pwani wakiangalia jengo ambalo Mwanafunzi huyo alikutwa amekufa baada ya kupotea kwa siku sita. Picha na Sanjito Msafiri

Kibaha. Imani za kishirikina zimetawala tukio la mtoto aliyetoweka kwa siku sita na baadaye mwili wake kukutwa ndani ya pagale ukiwa umeondolewa baadhi ya viungo.

Mwanafunzi huyo wa darasa la pili, Celina Fosi alitoweka siku ambayo alienda mnada wa Mwendapole mjini Kibaha akiwa na shangazi yake ambaye anafanya biashara maeneo hayo.

Waokota chupa waliona mwili wake kwenye jengo ambalo lilikuwa halitumiki na kutoa taarifa kwa wananchi walioenda kuutambua.

Shangazi mmoja wa Celina, Rosmely Haule, ambaye alitoka Dar es Salaam kwa ajili ya kuungana na ndugu zake kumsaka mwanafunzi huyo, alisema baada ya kupata taarifa waliripoti polisi ambao walifika eneo hilo na kukuta mwili wa marehemu ambao waligundua kuwa umekatwa baadhi ya viungo kama sehemu za siri, kitovu, nyama ya chini ya unyayo na kuchuna kichwani sehemu ya nywele,” alisema.

Sehemu nyingine zilizokutwa tofauti kwenye mwili wa marehemu huyo, kwa mujibu shangazi huyo, ni pamoja na kung’olewa meno, kukatwa masikio huku nguo yake ya ndani ikiwa imewekwa mdomoni mwake.

Alisema kuwa pia hali ilionyesha kuwa huenda marehemu alifanyiwa vitendo vya ubakaji kabla ya kuuawa kwa kuwa hali ilionyesha kulikuwa na msuguano eneo alilokutwa amekufa

“Mlangoni nje ya jengo hilo kulikuwa kumepangwa matofali na jirani na mwili wa marehemu tulikuta chupa tupu ya soda, pilipili za mwendokasi, vitunguu, matango na glovu za mipira,” alisema.

Kwa mujibu wa taarifa ya kamanda wa polisi wa Pwani, Wankyo Nyigesa aliyoitoa juzi, jeshi hilo lilipata taarifa hiyo na kufanya taratibu zinazostahili kisha kukabidhi mwili huo kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.

Kamanda Wankyo alisema Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka waliohusika ili hatua zichukuliwe na kutoa wito kwa wakazi wa Pwani kuwa waangalifu na watoto wao.

Kuhusu mazingira ya kupotea kwake, Agnes Peter, shangazi aliyekuwa akiishi na Celina, alisema siku hiyo walienda wote mnadani na baada ya muda akamshauri aende shule, lakini mtoto huyo akamjibu kuwa nguo zilikuwa hazijakauka.

Alisema baada ya muda aliomba ruhusa kwenda ndani ya mnada kutembea, lakini akamkatalia. Hata hivyo alisisitiza kwenda na ndipo alipomtoroka.

Alisema baada ya kugundua hali hiyo aliendelea na shughuli yake hadi alipomaliza ndipo alipoanza kumtafuta ndani ya mnada lakini hakufanikiwa na hivyo kuhisi kuwa alisharejea nyumbani.

“Lakini hata nyumbani sikumkuta ndipo nikatoa taarifa kwa ndugu wengine na majirani kuhusu tukio hilo na tukaanza kumtafuta na kueneza taarifa hiyo maeneo mbalimbali ikiwemo msikitini kwa ajili ya matangazo,” alisema.

Alisema siku hiyo hakufanikiwa na kesho yake walitoa taarifa polisi na kupewa RB ili kuendelea kumtafuta huku wakiamini kuwa wangempata akiwa mzima na wakawa wanakesha wakifanya maombi.

“Nilipata maelezo mengi lakini sikupata majibu,” alisema.

Mmoja wa majirani ambaye pia ni rafiki wa karibu na baba mzazi wa marehemu, Kiredio Mpeyi alisema alipata taarifa hiyo kutoka kwa waokota makopo.

“Nilikuwa napita njia nikakutana na waokota makopo wanakimbia nikawauliza kinachosababisha wanakimbia lakini hawakuwa tayari kusimama ili kunieleza zaidi ya kunielekeza niende kwenye jengo ili nijionee kilichomo ndani. Nilienda na nikakuta mwili wa marehemu huyo,” alisema.