Ushuru wa mazao mbioni kurejea nchini Tanzania

Muktasari:

Wizara ya Kilimo nchini Tanzania imewasilisha kwa Waziri wa Fedha na Mipango mapendekezo ya kurejesha ushuru wa  mazao katika Halmashauri nchini ili kuiwezesha Serikali kukusanya mapato kupitia sekta ya kilimo kwa mazao ya muda mrefu.

Korogwe. Wizara ya Kilimo nchini Tanzania imewasilisha kwa Waziri wa Fedha na Mipango mapendekezo ya kurejesha ushuru wa  mazao katika Halmashauri nchini ili kuiwezesha Serikali kukusanya mapato kupitia sekta ya kilimo kwa mazao ya muda mrefu.

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Septemba 27, 2019 na Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba baada ya wabunge na wenyeviti wa Halmashauri za Korogwe mji na vijijini kumlalamikia kuwa wazalishaji wa mkonge hawalipi ushuru huo na hivyo kuathiri makusanyo ya mapato.

Akizungumzia baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge nchini (TSB),  Yunus Msika kufafanua kuwa sheria haielezi kuhusu malipo ya mazao bali inaelekeza kuhusu malipo ya kodi ya huduma kwa viwanda.

Mgumba amesema baada ya kufanya vikao na mkuu wa Mkoa wa Tanga, wabunge na wakuu wa Wilaya zilizopo mkoani Tanga, kuzungumzia kuhusu kodi hiyo, Wizara hiyo iliamua kuwasilisha mapendekezo kwa waziri wa Fedha ili arejeshe kodi hiyo.

"Niwaombe mfanye subira, mapendekezo tayari yapo mezani kwa Waziri wa Fedha kwa kuwa kisheria yeye ndio mwenye mamlaka ya kukubali au kukataa, hivyo tufanye subira hadi mwakani,” amesema Mgumba.

Amesema hoja ya kurejeshwa kwa kodi ya ushuru wa mazao ina mashiko kwa kuwa hadi sasa mkoa wa Tanga unadai Sh9 bilioni za ushuru wa mazao kutoka mashamba mbalimbali ya mkonge katika Wilaya za Korogwe, Handeni- Pangani, Muheza na Mkinga.

Naibu waziri huyo yupo katika wilaya hiyo kukagua uzalishaji katika mashamba ya mkonge ili kuangalia changamoto zinazowakabili wazalishaji, hatimaye uzalishaji wa zao hilo uweze kuongezeka.

Uzalishaji wa mkonge nchini mwaka 2018 ulifikia tani 38,000.