Usifanye massage bila kufuata masharti haya

Muktasari:

Wataalamu wa afya wametoa angalizo kuhusiana na huduma ya kusingwa mwili ‘massage’ inayofanywa na watu katika maeneo mbalimbali nchini hasa mijini.

Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wametoa angalizo kuhusiana na huduma ya kusingwa mwili ‘massage’ inayofanywa na watu katika maeneo mbalimbali nchini hasa mijini.

Wamesema huduma hiyo inayoenea kwa kasi nchini, imekuwa ikitolewa bila kufuata hatua za kiafya ikiwamo kutambua historia ya afya ya anayehudumiwa jambo ambalo ni hatari.

Pasipo kufuata utaratibu huo, wameeleza kuwa upo uwezekano wa anayefanyiwa kupata athari zinazoweza kumsababishia maumivu ya kudumu au madhara makubwa zaidi.

Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam hivi karibuni, mtaalamu wa tiba ya mazoezi ya viungo wa Hospitali ya Rainbow, Dk Fortdas Lamila alisema, “mfano mtu mwenye saratani ya damu au kiungo chochote kilichoathiriwa na saratani hatakiwi kufanyiwa tiba hii maana itasababisha saratani kusambaa.”

“Mwili ukichuliwa unasababisha damu kuzunguka kwa kasi, hivyo ukiiruhusu ifanye hivyo kwenye eneo ambalo lina ugonjwa, ni rahisi kusambaa mwili mzima.”

Kauli hiyo imeungwa mkono na mtaalamu wa viungo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Abdalla Makalla ambaye ameeleza kuwa yapo madhara makubwa kiafya endapo ‘massage’ itafanywa bila kujua historia ya anayefanyiwa.

Pia, alisema mtu mwenye tatizo la damu kuganda na kutengeneza donge kwenye miguu linalofahamika kitaalamu kama Deep Vein Thrombosis (DVT), hatakiwi kufanyiwa huduma hiyo bila kupata ushauri wa daktari.

Mfanyakazi wa kituo cha ‘massage’ kilichopo katikati ya jiji, aliyejitambulisha kwa jina la Sekela alisema amefanya kazi hiyo kwa miaka mitatu, lakini hafahamu suala la kuzingatia historia ya anayefanyiwa.

Mmoja wa wateja katika kituo hicho ambaye hakutaka jina lake liandikwe alisema amekuwa akipatiwa huduma hiyo kwenye vituo mbalimbali, lakini hajui kama inaweza kuwa na athari.

Umewahi kusingwa mwili (massage) kwenye kituo au sehemu inayotoa huduma hiyo kwa ajili ya kuondoa uchovu lakini ukajiongezea maumivu?

Kama umekutana na hali hiyo, basi aliyekufanyia huduma hiyo siyo mtaalamu.

Kitabibu uchovu ni hali inayojitokeza pale misuli ya mwili inapofanyishwa kazi kupita kiwango chake kutokana na sababu mbalimbali hasa zinazotokana na maisha ya kila siku.

Mtaalamu wa tiba ya mazoezi ya viungo wa Hospitali ya Rainbow, Dk Fortdas Lamila anasema uchovu unaoambatana na maumivu ni njia mojawapo ya mwili kujihami na kukupa ishara kuwa viungo vya mwili hasa misuli imetumika kupita kiasi.

“Uchovu huu mara nyingi hutokea katika maeneo ya maungio, mfano mgongoni, kiunoni, mapajani na magotini.

“Mwathirika anaweza kuhisi pengine ana ugonjwa mkubwa kumbe tu ni uchovu wa viungo vya mwili.

“Uchovu huu wakati mwingine unaweza kusababisha misuli ya mwili kukosa nguvu kama ilivyo kawaida yake. Tatizo hili linaweza kuambatana na maumivu yanayoweza kuwa ya wastani mpaka kuwa makali,” anasema.

Katika maeneo ya mijini baadhi ya watu wakiwa katika hali hiyo hukimbilia kwenye vituo vya kusinga (massage centres) au kwa watu wanaoweza kuwapatia kuwachua miili kwa lengo la kupata unafuu.

Nani anapaswa kutoa huduma?

Lakini wataalamu wanasema si kila mtu anaweza kutoa huduma hii kwa kuwa inahitaji utaalamu wa hali ya juu kinyume na hapo inaweza kumsababishia mhusika madhara makubwa kiafya.

Dk Lamila anasema kazi ya kuchua misuli inatakiwa kufanywa na mtu mwenye utaalamu na anayeweza kutambua ni mishipa ipi ya fahamu katika mwili wa binadamu haitakiwi kusingwa na wapi panastahili kupewa huduma hiyo.

“Kama ilivyo matibabu mengine haya pia yanapaswa kutolewa na mtu ambaye amebobeba na ana utaalamu wa kutosha, ndiyo maana hospitali kuna vitengo maalumu na wapo watu wamesomea huduma hii wakiifanya kwa kuzingatia vigezo maalumu.

“Kuna sehemu za mishipa ya fahamu ukizigusa zinaweza kuleta matatizo makubwa kwa mhusika hasa inapotokea anayefanya huduma hiyo akashindwa kuzingatia ni aina gani ya tiba mgonjwa anahitaji,”anasema Dk Lamila.

Pia, anasema zipo aina tatu za ‘massage’ ambazo ni kawaida (soft) inayoondoa uchovu, kati (medium) yenye mchanganyiko wa kuondoa uchovu na kuchua misuli kidogo na hard (ngumu) kwa ajili ya kuchua misuli na hii inafanywa zaidi kwa wanamichezo.

“Aina zote hizo zina kazi zake na sababu za kufanywa kwenye mwili wa binadamu. Mfano mtu anayehitaji soft akifanyiwa hard itamletea madhara na bahati mbaya wasio wataalamu wanaishia kuchanganya aina hizi,” anafafanua daktari huyo.

Kwanini ufanywe ‘massage’

Dk Lamila anasema kabla ya kumpatia mtu huduma hiyo, lazima mtoaji afahamu sababu ya mhusika kuhitaji tiba na nini hasa kinamsumbua.

Anasema mtaalamu wa kuchua, lazimia achukue historia ya kiafya ya muhusika na shughuli anazofanya.

Dk Lamila anasema endapo muhusika atakuwa na tatizo lolote la kiafya au kama kuna matibabu yoyote anaendelea nayo itakuwa rahisi kwa mtaalamu kujua ni aina gani ya ‘massage’ amfanyie.

“Ukishajua yote hayo ndio itakuwa rahisi kuelewa ni aina ipi inamfaa lakini wengi wanahitaji ‘soft massage’ kwa ajili ya kuondoa uchovu na ikitokea ana maumivu inaweza kwenda hadi kwenye ‘medium.’

“Mfano mtu mwenye saratani ya damu au kiungo chochote kilichoathiriwa na saratani hatakiwi kufanyiwa tiba hii maana itasababisha saratani kusambaa.

“Mwili ukichuliwa unasababisha damu kuzungua kwa kasi, hivyo ukiiruhusu ifanye hivyo kwenye eneo ambalo lina ugonjwa ni rahisi kusambaa mwili mzima.

“Kwenye pingili za mgongo na tumboni pia hakutakiwi kufanyiwa tiba hiyo kutokana na muundo wake,” anasema.

Dk Lamila anasema ‘hard massage’ hufanywa kwa wanamichezo na ikitokea mtu wa kawaida akafanyiwa inaweza kuumiza misuli yake na matokeo yake kupata madhara yanayoweza kumletea ugonjwa.

Hilo linaungwa mkono na Mfizotherapia wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Abdalla Makalla anayeeleza kuwa yapo madhara makubwa kiafya endapo ‘massage’ itafanywa bila kujua historia ya anayefanyiwa.

Hata hivyo, Dk Makalla anasema zipo aina mbili za ‘massage’ moja ikiwa ni ile ya tiba na nyingine ya kuondoa uchovu.

Mtaalamu huyo anasisitiza kuwa kama mtu hujafanya vipimo vya afya na kujua kwa kina hali yake, usijaribu kufanya tiba hii kwa kuwa inaweza kuleta madhara mwilini.

Anasema, “Ikitokea mtu shinikizo lake la damu limepanda asije kukimbilia kufanya ‘massage’ akifikiri ndiyo atapata unafuu hiyo itamletea athari zaidi.

“Hii ina maana kwamba presha ikiwa juu halafu ukaifanya damu iende kwa kasi ni kuongeza tatizo juu ya tatizo,” anasema Dk Makalla.

Pia, anaeleza kuwa mtu mwenye tatizo la damu yake kuganda na kutengeneza donge la damu kitaalamu inafahamika kama DVT Deep vein thrombosis, naye anatakiwa kujiweka kando na huduma hii.

Ikitokea mtu mwenye tatizo hilo akafanyiwa ‘massage’ kuna uwezekano wa bonge hilo kusafirishwa na kwenda katika sehemu nyingine ambazo hazitakiwi kuzibwa kama kwenye moyo au mapafu.

“Pia kama mtu mwenye saratani ya aina yoyote atakiwi kujihusisha na hilo kwa kuwa ataifanya isambae hata katika maeneo ambayo ilikuwa haijafika na hilo litamfanya siku zake za kuishi kupungua kutokana ugonjwa kusambaa mwilini kwa kasi,” anasema Dk Makalla

Mtaalamu huyo wa afya anasema watu wenye matatizo ya mgongo, kiharusi na watoto wenye mtindio ni muhimu kufanyiwa mazoezi kwenye vituo maalumu ambavyo vina wataalamu kwa ajili ya kazi hiyo na si vinginevyo.

“Kuna watu mitaani huko wanadai kwamba wanawafanyia ‘massage’ kunyoosha viungo hasa kwa watoto wenye mtindio au wagonjwa wa kiharusi, niwaleze wazi kuwa kazi hiyo inafanywa na wataalamu tu, hao wa mitaani wanaongeza mkakamao,” anasema.