Utaratibu mpya kusaka washiriki Miss Tanzania 2020

Muktasari:

Kamati ya Miss Tanzania imeachana na utaratibu wa zamani wa mawakala kutafuta washiriki wa shindano hilo na badala yake itazunguka katika kanda zote nchini kuwafanyia usahili.

Dar es Salaam. Kamati ya Miss Tanzania imeachana na utaratibu wa zamani wa mawakala kutafuta washiriki wa shindano hilo na badala yake itazunguka katika kanda zote nchini kuwafanyia usahili.

Utaratibu huo mpya wa kutafuta warembo watakaoshiriki mashindano ya Miss Tanzania unatarajiwa kuanza Machi, 2020.

Akizungumza leo Alhamisi Februari 27, 2020 Mkurugenzi wa kamati hiyo, Basila Mwanukuzi amesema utaratibu huo utasaidia  kuondoa changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwa baadhi ya mawakala ambao hawakuwa waaminifu.

Amezitaja changamoto hizo kuwa ni kusimamia warembo, utoaji wa zawadi, kujaza na urudishaji  fomu kwa wakati ili warembo waweze kufanyiwa usahili.

“Usahili utaanza Kanda ya kati Machi 7 jijini Dodoma, Kanda ya Kaskazini Machi 14, Kanda ya Ziwa Machi 28, Kanda ya Mashariki Aprili 4. Kanda ya vyuo vikuu Aprili 21, Kanda ya nyanda za juu Kusini Aprili 11 na Kanda ya Dar es Salaam itakuwa Mei 2, 2020,”amesema mkurugenzi huyo katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Amesema Miss Tanzania mwaka 2020 itajikita  kutangaza misitu na utalii wa asili, uhamasishaji wa kupanda miti katika kila kanda.