Utata anayedaiwa kujinyonga akiwa amevaa gauni la mkewe

Saturday November 9 2019

 

By Daniel Makaka, Mwananchi [email protected]

Buchosa. Msemakweli Zikiliza (31), mkazi wa wilayani Sengerema amejinyonga hadi kufa na mwili wake kukutwa ukining’inia katika mti wa mwembe.

Tukio hilo limetokea kijiji cha Mwabasabi kata ya Nyehunge mkoani Mwanza usiku wa kuamkia jana Ijumaa Novemba 8, 2019.

Tukio hilo ni la pili ndani ya mwezi mmoja na nusu katika wilaya hiyo kwani Septemba 25, 2019 Mashaka Zakaria (26) alijinyonga hadi kufa huku rafiki yake akidai alichukua uamuzi huo baada ya kumkuta mpenzi wake akicheza muziki na mwanaume mwingine.

Akizungumza na Mwananchi Kefline Patrick, ambaye ni mke wa Zikiliza amesema mumewe aliondoka nyumbani juzi usiku Alhamisi Novemba 7, 2019 kwenda kwenye matembezi na aliondoka na gauni lake kwa maelezo kuwa analipeleka kwa fundi kushonwa kwa kuwa lilikuwa limefumuka nyuzi.

Kefline amesema jana asubuhi wakati akielekea katika shughuli zake alipita kando ya mti huo na kukuta mwili wa mumewe ukining’inia.

“Alikuwa amevaa gauni langu kwa kweli siamini kilichotokea,” amesema Kefline.

Advertisement

Ofisa mtendaji wa kata hiyo, Edimundi Gerevas amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, akibainisha kuwa chanzo hakijajulikana. Amesema amepata taarifa hizo kutoka kwa mke wa Kefline.

Mkuu wa polisi wilaya ya Sengerema, Maili Makori amesema polisi wanaendelea na uchunguzi, hakuna anayeshikiliwa akihusishwa na tukio hilo.

 

Advertisement