Utata anayedaiwa kukatwa mkono baada ya kumfumania mkewe

Wednesday February 19 2020

By Anthony Mayunga, Mwananchi [email protected]

Serengeti. Paul Marwa (25), mkazi wa kijiji cha Gwikongo kata ya Mbalibali Wilaya ya Serengeti amekatwa mkono wa kushoto na mtu anayedai kuwa alimfumania akiwa na mkewe nyumbani kwake.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Februari 19, 2020 mganga mkuu wa Hospitali ya Nyerere, Tanu Warioba amesema Marwa amepewa rufaa kuonana na daktari bingwa wa mifupa mjini Musoma.

"Tumempokea Jumanne usiku Februari 18, 2020. Mkono wake ulikuwa unaning'inia umeshikwa na ngozi tu nikalazimika kumpa rufaa maana sisi hatuna mabingwa wa mifupa ,ameondoka asubuhi ya leo kwenda huko," amesema.

Akisimulia mkasa huyo daktari huyo amesema Marwa alimueleza kuwa aliporudi nyumbani kwake alimkuta mkewe akiwa na mwanaume chumbani na katika purukushani mwanaume huyo alichukua panga na kumkata mkono.

Hata hivyo, mtendaji wa serikali ya kijiji hicho, Vumilia Gitano amesema habari alizonazo Marwa alikakatwa mkono baada ya kukutana na mwanaume huyo njiani.

“Aliporudi nyumbani hakumkuta mkewe, na mkewe  aliporudi alianza kumpiga akidhani alikuwa kwa huyo mwanaume. Baada ya kumpiga alitoka kwa lengo la kumtafuta huyo mwanaume na wakakutana njiani.”

Advertisement

“Katika kulumbana ndipo alipokamatwa mkono. Hivyo ndivyo nilivyoelezwa na wananchi niliozungumza nao,” amesema mtendaji huyo wa kijiji

Amesema kwa sasa wanamsaka mtuhumiwa huyo kwa ajili ya hatua zaidi.

Advertisement