Uturuki kutuma vikosi vya jeshi Libya

Rais wa Uturuki Reccip Tayyip Erdogan

Muktasari:

Serikali ya Libya yaomba msaada wa kijeshi ili kuwadhibiti waasi.

Istanbul. Rais wa Uturuki Reccip Tayyip Erdogan amesema serikali ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imeiomba nchi yake kupeleka vikosi vya jeshi kuulinda mji mkuu Tripoli dhidi ya mashambulizi ya waasi.

Kufuatia ombi hilo, Erdogan amesema Bunge la Uturuki litajadili na kupiga kura mwezi Januari kuamua kuhusu ombi hilo.

Akizungumza na maofisa wa chama tawala, Erdogan amesema serikali ya mjini Tripoli inayoongozwa na Waziri mkuu  Fayez Sarraj imeikaribisha Uturuki kutuma vikosi vyake chini ya makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi yaliyotiwa saini hivi karibuni na pande hizo mbili.

Utawala wa Sarraj umekabiliwa na uchokozi tangu mnamo Aprili kutoka serikali hasimu ya upande wa mashariki na vikosi vinavyoongozwa na Jenerali muasi Khalifa Haftar, ambaye anajaribu kuchukua udhibiti wa mji mkuu, Tripoli.

"Tutakwenda maeneo tuliyokaribishwa na hatutokwenda kwenye maeneo ambayo hatukualikwa," amesema Erdogan na kuongeza kwa kuwa Libya imetoa mwaliko huu, Uturuki itauridhia na kutuma vikosi vyake.

Erdogan amesema nchi yake itatoa msaada unaohitajika kwa serikali ya Libya dhidi ya kitisho cha jenerali Haftar anayelenga kufanya mapinduzi ya kijeshi akiungwa mkono na mataifa kadhaa ya Ulaya na ya Kiarabu.

"Tuko upande wa serikali halali ya Libya" ameongeza Erdogan.

Kiongozi huyo amesema muswada wa sheria kuidhinisha hatua hiyo utaweza kupelekwa bungeni kati ya Januari 8 au 9 baada ya wabunge kurejea kutoka mapumziko ya mwisho wa mwaka.

Ni wazi muswada huo utaidhinishwa na Bunge

Chama cha Rais Erdogan kina idadi kubwa ya wabunge, hali inayoashiria kuwa muswada huo utaidhinishwa na Bunge bila pingamizi.