Uuzaji nyumba NHC, NIC kuchunguzwa

Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameiagiza ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI)kuchunguza nyumba ya Shirika la Bima (NIC) iliyouzwa kwa Sh100 milioni wakati ina thamani ya zaidi ya Sh1.2 bilioni.

Nyumba hiyo ipo Kitalu 459 mtaa wa Chalambe upanga,wilayani Kinondoni.

Sambamba na hilo, ameagiza ofisi hiyo kuchunguza uuzaji wa nyumba kwa aliyekuwa mpangaji wa Shirika la Nyumba la Taifa(NHC) iliyopo mtaa wa Ursino Kata ya Mikocheni, wilayani Kinondoni.

Lukuvi alitoa maagizo hayo jana alipofanya ziara katika nyumba hizo akiwa ameongozana na Naibu Kamishna wa Polisi kutoka ofisi ya DCI, Afwilile Mponi.

Akizungumzia nyumba ya NHC, Waziri Lukuvi alisema mpangaji aliyetajwa kwa jina la Charles Sakodia, alipangishiwa na kampuni yake miaka 15 iliyopita,lakini baadaye aliingia mkataba na kuuziwa nyumba hiyo na kueleza kuwa haieleweki ilikuwaje.

“Miezi miwili iliyopita baada ya kugundua kwamba mpangaji huyu kauziwa nyumba hii isivyo halali niliwaambia NHC wafuatilie na kuirudisha,lakini naona kazi hii wameshindwa,” alisema na kuongeza:

“Hivyo nimeamua kukabidhi suala hilo kwa DCI ashughulike, kwani hata makaratasi ya mkataba ukiangala alivyouziwa yanatia utata, mwenyewe nilipomtaka alete nyaraka hakuwa nazo.”

Kwa nyumba ya NIC, alisema kikubwa anachotaka kichunguzwe ni kwa nini baada ya kuwekwa zuio na mahakama bado nyumba hiyo ikauzwa.

“DCI usiwaonee aibu watu katika uchunguzi huu, najua hata wa ofisini kwangu wanahusika katika hili,” alisema.

Awali akielezea sakata la nyumba hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Elirehema Doriye, alisema ilipigwa mnada baada ya mwaka 1996 mteja wao kufungua kesi ya madai.

Hata hivyo, alisema Septemba 2006 shirika lilipa fedha inayodaiwa na mahakama ya Kisutu iliyokuwa ikisikiliza kesi hiyo iliwapa risiti na kueleza kushangaa Oktoba 29 nyumba ilipigwa mnada na kununuliwa na kampuni ya Import and Export inayomilikiwa na mtualiyemtaja kwa jina la Hans Macha.