VIDEO: Familia yasubiri DNA kuweka msiba

Dar es Salaam. Pamoja na familia ya Naomi Marijani kugubikwa na simanzi baada ya taarifa ya polisi kudai kuwa mumewe Khamis Luwongo anahusika kumuua, itailazimu kusubiri kwa siku kati ya tano hadi 10 kuweka msiba.

Muda huo utakuwa wa kusubiri majibu ya kipimo cha vinasaba (DNA) kilichochukuliwa kwenye mabaki ya mwili unaodaiwa kuwa ni wa Naomi ambavyo vitalinganishwa na vya kaka yake.

Naomi (36) alipotea nyumbani kwake Mei 15 na siku nne baadaye, mumewe alitoa taarifa kwa familia na ndugu wa mkewe kuhusu kutoweka huko.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Amon Kakwale alisema jana kuwa Luwongo (38) anadaiwa kukiri kumpiga na kumuua mkewe kisha kuuweka mwili kwenye shimo alilolichimba ndani ya banda la kufugia kuku.

Baada ya kuuweka kwenye shimo hilo, Luwongo anadaiwa kuchukua magunia mawili ya mkaa na mafuta ya taa kisha kuuchoma moto na alipomaliza anadaiwa kwamba alichukua majivu na kwenda kuyafukia kwenye shamba lake lililopo Kijiji cha Mlogolo kata ya Vikindu, Wilaya ya Mkuranga.

“Alichimba shimo kwenye shamba lake kisha kuweka hayo majivu na kufukia na akapanda mgomba juu yake. Mei 19 akafungua jalada polisi akidai mkewe ametoroka nyumbani na Juni 12, alifungua jalada lingine akimtuhumu mkewe kumtelekezea mtoto,” alidai Kakwale.