VIDEO: Jinsi ajali ilivyoua vigogo watano TRC

Dar/Tanga. Wakati nchi ikiwa katika vita dhidi ya kuenea kwa ugonjwa wa virusi vya corona unaoua maelfu ya watu duniani, Shirika la Reli (TRC) limepoteza maofisa wake watano waandamizi baada ya mabehewa kugongana na kiberenge kilichowabeba maofisa hao.

Wakati TRC ikianza uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo, Jeshi la Polisi limeeleza jinsi ilivyotokea.

Ajali hiyo imehusisha treni ya uokoaji iliyogongana na kiberenge kati ya stesheni za Mwakinyumbi na Gendagenda katika reli ya Dar-Kilimanjaro na kusababisha vifo vya watumishi hao, wakiwamo mameneja watatu.

Huduma za usafirishaji abiria katika reli hiyo zilirejea mwishoni mwa mwaka jana baada ya kusimama kwa miaka 25, lakini ajali ya juzi haikuhusisha treni ya abiria.

Wafanyakazi sita wa TRC walikuwa katika ajali hiyo, kwa mujibu wa Jamila Mabrouk ambaye ni mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa TRC. Wanne walifariki papo hapo wakati wawili walipelekwa hospitali na mmoja akafariki dunia baadaye.

“Wanne walifariki palepale eneo la ajali na majeruhi wawili walifikishwa hospitali ya wilaya ya Korogwe (Magunga) kwa huduma za kitabibu,” alisema Mabrouk.

“Mpaka ilipofikia saa 5:00 usiku Machi 22, 2020, majeruhi mmoja alifariki na kufikia jumla ya watano waliofariki.”

Waliofariki katika ajali hiyo ni Ramadhani Gumbo, ambaye ni meneja usafirishaji Kanda ya Tanga, Fabiola Mushi (meneja ukarabati wa mabehewa ya abiria wa Kanda ya Dar es Salaam) na Joseph Komba (meneja msaidizi wa usafirishaji Kanda ya Dar es Salaam).

Wengine ni mtaalamu wa usalama wa reli, Philbert Kajuna na dereva wa kiberenge, George Urio.

Taarifa hiyo imesema hadi sasa, Elizabet Bona, ambaye ndiye majeruhi aliyesalia na ambaye ni muongozaji treni, anaendelea na matibabu katika hospitali hiyo.

“Aidha uchunguzi wa kujumuisha taasisi nyingine utafanywa kubaini chanzo cha ajali hii hiyo,” imesema taarifa hiyo ya TRC jana.

Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Mohamed Athuman, ambaye ni mkazi wa kitongoji cha Mgongola, aliliambia Mwananchi kuwa aliona mabehewa yakirudi nyuma bila kuwa na kichwa cha treni na kugonga kiberenge hicho.

Kaimu kamanda wa polisi wa mkoa wa Tanga, Leons Rwegasira alisema ajali hiyo ilitokea katika Kitongoji cha Mgongola B, Kijiji cha Kwadoya wilayani Handeni.

Alisema Alhamisi iliyopita treni iliyokuwa ikitoka Tanga kwenda mkoani Pwani ikiwa imepakia saruji, ilipata ajali na mabehewa matano yalianguka katika kitongoji hicho.

“Jana (juzi) wafanyakazi wa TRC walikwenda eneo la tukio kwa lengo la kushusha mizigo, kuisafirisha kwa kutumia mabehewa mengine na kuyainua yaliyoanguka,” alisema kamanda huyo.

“Katika harakati za kupakua walipokamilisha kazi ya kuondoa shehena yote ndani ya mabehewa, walifanikiwa kuyainua na kuyaweka katika njia yake, ndipo mabehewa yakaanza kurudi nyuma.

“Kiberenge kilikuwa kinakwenda eneo la ajali, sasa mabehewa yalivyonyanyuliwa yakaanza kurudi nyuma na kukutana na kiberenge kikiwa kinakwenda eneo hilo na kugongana.”

Taratibu za mazishi

Kuhusu waliofariki, mkuu wa kitengo cha usalama wa reli wa TRC, Maizo Mgezi alisema wamekamilisha taratibu zote za kitabibu na walianza safari kwa ajili ya kupeleka miili ya waliofariki jijini Dar es Salaam ili kuwezesha familia zao kuichukua.

“Tunatarajia kuanza safari jioni hii (jana) na miili ya marehemu itahifadhiwa Hospitali ya Lugalo. Hatutakuwa na hafla ya kuaga kwa pamoja kutokana na ugonjwa wa corona kuzuia mikusanyiko,” alisema.

“Familia za marehemu zitahusisha watu wachache wakati wa kuchukua miili ya wapendwa wao.”

Licha ya treni kutumia njia moja, kwa kawaida ajali baina ya treni hutokea kwa nadra kutokana na mifumo yake ya uongozaji vyombo hivyo vya usafiri vinavyochukua idadi kubwa ya abiria na mizigo.

Taakriban miaka 11 iliyopita, ajali iliyohusisha treni kwa treni ilitokea eneo la Msagali wilayani Mpwapwa iliyosababisha watu 13 kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa vibaya.

Ajali hiyo ilisababishwa na kitendo cha treni ya mizigo iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda Mwanza kusimama eneo hilo bila ya kuwepo taarifa. Kama ilivyokuwa katika ajali ya juzi, mabehewa ya abiria yalichomoka na kurudi nyuma hadi eneo ilipokuwepo treni ya abiria na hivyo kugongana.

Abiria waliofariki na kujeruhiwa waliumia kutokana na mabehewa hayo kukatika na kuwabana na mengine kuanguka.

Ajali nyingine za chombo hicho kinachotembea katika njia maalum, huhusisha treni na magari.