VIDEO: Mtanzania asimulia madhila ya corona Italia

Wednesday March 25 2020

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. “Wakati ugonjwa huu umeingia Italia na kushuhudia namna watu wanavyopoteza maisha, nilimwomba sana Mungu tatizo hili lisifike nyumbani Tanzania kwa kuwa nafahamu hali zetu, mfumo wetu wa maisha na huduma za afya, sikutaka kabisa Watanzania wapate janga hili.”

Ni maneno ya Mtanzania Rose Maenda anayeishi nchini Italia katika Jiji la Rome.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) Italia ni nchi iliyoathirika zaidi katika bara la Ulaya kutokana na ugonjwa wa corona ambapo hadi sasa watu zaidi ya 64,000 wameambukizwa na zaidi ya 6,000 wamepoteza maisha.

Rose anasema licha ya kuwa Italia ni nchi iliyoendelea ikiwa na mfumo mzuri wa utoaji wa huduma za afya, ugonjwa huo umewashinda kutokana na kasi ya maambukizi kuwa kubwa.

Rose anasema kosa kubwa ambalo liliwaponza watu wa nchi hiyo ni kudharau ugonjwa huo ulipoingia na kuendelea na maisha yao kama kawaida, jambo lililosababisha ugonjwa kusambaa na kuleta athari kubwa.

“Waitaliano ni watu wenye upendo na wanapenda mikusanyiko, masuala ya kukumbatiana, kushikana mikono ni vitu vya kawaida, ndiyo maana ugonjwa ulipoingia ukatupiga namna hii,” aliongeza Maenda.

Advertisement

Anasema mfumo wa maisha ya Waitaliano hauna tofauti sana na ule wa Watanzania kwa watu kupenda kuchangamana, jambo ambalo limekuwa likimtia hofu endapo ugonjwa huo utasambaa zaidi.

“Nafuatilia taarifa na kuona hali inavyoendelea Tanzania naumia kuona watu wanachukulia poa huu ugonjwa, jamani naomba tulichukulie hili suala kwa uzito, huu ugonjwa ni hatari watu wanapoteza maisha. Tumelia hadi imefika wakati nimezoea.

“Inauma sana kuona rafiki, ndugu na jamaa anapoteza maisha halafu huwezi kumzika kwa hali iliyofikia Italia, maiti hawazikwi wanachomwa moto, hivyo hata majivu huoni. Inasikitisha kila ninapoangalia runinga na vyombo vya habari ni watu wamekufa sitamani kuliona hili Tanzania. Watu wachukue tahadhari kubwa tujizuie kuchangamana na kufuata maelekezo ya wataalamu.

“Mjitahidi kukaa nyumbani kwa kuwa ndiyo sehemu salama, maana hata kama unanawa mikono halafu bado unazurura barabarani hiyo ni kazi bure bado unajiweka kwenye mazingira hatarishi,” anaonya Maenda.

Maisha yakoje kwa sasa

Anasema kwa sasa kuna amri ya watu wote kutotoka nje ya makazi yao na wanaokiuka maelekozo hayo hukamatwa na kufungwa jela.

“Leo ni siku ya 15 hakuna kwenda kazini wala kwenye shughuli yoyote, wanaofanya kazi kwa sasa ni watu wa sekta ya afya, polisi na wanajeshi. Ukipita mtaani polisi lazima wakuhoji sababu za kuwepo nje na kama hazina msingi unafungwa.

“Kwenye nyumba anaruhusiwa kutoka mtu mmoja kwa ajili ya kwenda kufuata mahitaji muhimu kama chakula na dawa, lazima awe amevaa mavazi ya kujikinga na kama ni madukani kuna utaratibu mtu akifika anapanga foleni kwa kuachiana mita moja,” anaeleza.

Advertisement