VIDEO: Sheikh apotea siku nne, maiti yake yakutwa ofisini

Dodoma/mikoani. Sikukuu ya Krisimasi ilihitimishwa jana. Wapo waliosherehekea kwa kula, kunywa na kuburudika kwa muziki, lakini kwa baadhi ilikuwa majonzi baada ya kupoteza wapendwa wao.

Matukio ya vifo vya watu watano vilivyotokea Arusha, Dodoma na Mara yametia doa sikukuu hiyo na kuwa simanzi katika maeneo mbalimbali nchini.

Kifo cha Sheikh Rashid Bura ambaye ni mmiliki wa Shule za Zam Zam mkoani Dodoma ambaye alikutwa amefariki ofisini kwake baada ya kupotea kwa siku zaidi ya nne, na lile la Moses Pallangyo mkazi wa Arumeru mkoani Arusha anayetuhumiwa kumuua kwa kumkata shoka mkewe, Marry Richard Mushi yameacha majonzi.

Sikukuu hiyo inayoadhimishwa na Wakristo kila mwaka kusherekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo, pia ilihitimishwa kwa kushuhudia watoto wawili wa familia moja ya Serengeti mkoani Mara wakifikwa na mauti baada ya kuangukiwa na nyumba huku dereva bodaboda wilayani humo akisombwa na maji na kupoteza maisha.

Tukio la mmiliki wa shule za Zam Zam, Sheikh Bura (60) limezua hofu baada ya kutoonekana kwa siku zaidi ya nne kisha juzi alasiri akakutwa amefariki ofisini kwake eneo la Majani ya Chai karibu na bustani ya Nyerere Square, katikati ya jiji la Dodoma. Mwili wake ulizikwa jana saa saba mchana katika makaburi ya Chamwino.

Maziko ya Bura yalihudhuriwa na kamanda wa polisi wa mkoa, Gilles Muroto, Sheikh wa mkoa, Mustapha Rajabu na baadhi ya maprofesa wa Chuo Kikuu cha Dodoma.

Bura mbali na uanaharakati wa kutetea haki za binadamu pia ni polisi mstaafu ambaye aliwahi kuwa mlinzi wa getini Ikulu jijini Dar es Salaam kwa miaka mitatu mfululizo na pia aliwahi kuwa ofisa upelelezi wa makosa ya jinai (CID).

Akizungumza na Mwananchi baada ya maziko, Ali Rashid Bura (26), mtoto wa marehemu, alisema alifika juzi ofisini kwa baba yake akiwa katika harakati za kumtafuta baada ya kutoonekana kwa siku nne.

Alisema, juzi siku ya Sikukuu ya Krismasi, alitoka Kituo kikuu cha polisi ambako aliongozana na rafiki wa marehemu kwa ajili ya kufungua jalada la uchunguzi, ndipo akakuta milango ya ofisi imefungwa, huku kukiwa na harufu kali kutoka ndani ya ofisi.

“Tulianza kumtafuta tangu Jumanne, tulitoa taarifa polisi, lakini jana (juzi) majira ya saa 11:00 jioni niliachana na wenzangu, nikaenda ofisini kwake. Nilichokikuta dah,” alisema Ali huku akifuta machozi.

Akielezea kuhusu ofisi hiyo ambayo ipo ghorofani, alisema alikuta mlango wa kwanza wa geti ukiwa umerudishiwa lakini alipousukuma ulifunguka ikatoka harufu kali ndani wakati mlango wa pili ambao ni wa mbao ulikuwa umefungwa.

“Nilikuwa na ufunguo mmoja, nilijaribu kufungua haukufunguka ndipo nikaenda kuwaambia ofisi ya pili wakasema walishaanza kusikia harufu siku mbili zilizopita. Hakukuwa na namna nikaenda kuupiga teke mlango ukafunguka ndipo nikauona mwili wa baba ukiwa umeharibika sana huku akiwa amekaa chini na nguo zote zikiwa pembeni,” alisema.

Alisema simu yake ilikuwa imezimwa, iliwekwa pembeni pamoja na begi alilosafiri nalo likiwa na fedha, jambo ambalo limemfanya aamini hakukuwa na kitu kilichochukuliwa labda kama ni nyaraka.

Kwa mujibu wa Ali, hana taarifa kama baba yake alikuwa na ugomvi na mtu zaidi ya kuwaaga kuwa alikuwa akienda jijini Dar es Salaam.

Msemaji wa familia

Msemaji wa familia, Abdillah Mboryo alisema Sheikh huyo aliaga kwamba anakwenda Dar es Salaam Ijumaa ya Desemba 20, kuhudhuria mkutano wa amani.

Mboryo alisema kulikuwa na mawasiliano na rafiki yake hadi Jumapili jioni alipokuwa amerudi Dodoma kwa usafiri wa basi.

Rafiki huyo ambaye wameanzisha pamoja taasisi ya Dalai Islamic Center kwa ajili ya kupeleka Waislamu Hijja, alisema familia ya marehemu ilimpa taarifa kwamba hawamuoni Bura wala simu yake haipatikani.

“Tulipeleka taarifa kwa kamanda wa polisi mkoa (Muroto) maana ni rafiki yake wa karibu na walifanya kazi pamoja wakiwa polisi,” alisema.

“Ndipo akatushauri tukafungue jalada kituo kikuu cha polisi na kisha tukaenda kumueleza Sheikh wa mkoa (Mustapha Rajabu).

“Mwili wa marehemu ulikuwa na majeraha matatu; mkono wa kushoto, kwenye paja na mgongoni ambayo siwezi kuyazungumzia kwa sababu mimi si polisi lakini niliyaona,” alisema Mboryo.

Hata hivyo, alikanusha taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa alikutwa amekatwa sehemu za siri, akisema macho yake yalimshuhudia akiwa salama pamoja na kuwa hakuwa na nguo.

Muroto kimya

Kama ilivyokuwa juzi, jana pia Kamanda Muroto alifika nyumbani kwa marehemu eneo la Chang’ombe Extension akiongozana na gari la polisi lililobeba mwili wa marehemu, lakini hakuwa tayari kuzungumza chochote.

Muroto alishiriki hata mazishi ya Bura kwa kuweka udongo katika makaburi ya Chamwino Jijini hapa huku kukiwa na magari mengi ya polisi yaliyoegeshwa katika viwanja vya Shule ya Msingi Chinangali.

Lakini sheikh wa mkoa, Mustapha Rajabu alisema aliwasiliana na Bura Jumapili jioni akimweleza kuhusu safari yake na kuwa alikuwa amerudi salama.

Alisema Bura alimpigia simu na ilikuwa kawaida yake kila mara kueleza kile alichotumwa kukifanya kama sehemu ya mrejesho.

Mustapha aliliambia Mwananchi kuwa alimteua Bura kutokana na uwezo wake na historia yake katika masuala ya ulinzi na amani, na wajibu wake ulikuwa kuwawakilisha Waislamu kwenye mkutano huo.

Alisema Bura alikuwa mwanaharakati wa mfano asiyetiliwa shaka katika kuwasaidia Watanzania walio Waislamu na wasiokuwa Waislamu kwa kuwa hakupenda kuona mtu anaonewa.

Kwa mujibu wa sheikh huyo, Bura alikuwa ni miongoni mwa washauri wake wa siri katika mambo mengi na makubwa hivyo akasema itamchukua muda kumpata mtu kama huyo.

Jengo la ofisi yake

Watu wanaofanya kazi kwenye jengo lenye ofisi ya mkurugenzi huyo wa Dalai Islamic Center, wamesema mara ya mwisho kuonana na Bura ilikuwa Jumapili ya Desemba 22, saa 10:00 jioni.

Akizungumza na gazeti hili fundi wa kuchonga mihuri anayefanyakazi katika eneo la jengo hilo Hiari Jacob alisema mara ya mwisho kuonana na marehemu ilikuwa Desemba 22 wakati akiingia ofisini kwake na kutoka.

Alisema baada hapo hawakuonana tena mpaka Desemba 25 siku ya Sikukuu ya Krismasi alipokuja kijana wake aliyemtaja kwa jina la Ali na kumuulizia.

Alisema walimwambia kuwa huenda amesafiri, lakini kijana huyo akawajibu kuwa hawezi kusafiri bila kumuaga mama yake na ndipo akapandisha juu ofisini kwa baba yake.