VIDEO: Banda, Kichuya waikosa AFCON, Yussuf aula

Muktasari:

Taifa Stars iliyopangwa Kundi C katika Fainali za AFCON, itafungua dimba dhidi ya Senegal na baadaye itaikabili Kenya kabla ya kumalizia na Algeria.


Cairo, Misri. Wakati benchi la ufundi la timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ likitoa orodha ya mwisho ya wachezaji 23 watakaoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), kiungo mshambuliaji Shiza Kichuya, beki kiraka Abdi Banda na mshambuliaji Shaban Chilunda ni miongoni mwa nyota tisa walioenguliwa kikosini.

Licha ya kuteuliwa kwenye kikosi cha awali, watatu hao wanaocheza soka la kulipwa katika nchi za Hispania, Afrika Kusini na Misri wameshindwa kupenya kwenye kikosi cha wachezaji 23 ambao kikanuni ndio watashiriki fainali hizo.

Kocha Emmanuel Amunike ameshindwa kumjumuisha Banda  anayecheza Baroka FC ya Afrika Kusini na badala yake ameamua kuwajumuisha kundini Ally Mtoni 'Sonso' wa Lipuli na nyota wa Mbao FC, Vincent Philipo.

Kwa upande wa Kichuya anayecheza ENPPI ya Misri, ameshindwa kufua dafu mbele ya Farid Mussa, Thomas Ulimwengu na Yahya Zayd.

Hakukuwa na nafasi kwa mshambuliaji Shabani Chilunda ambaye hivi karibuni amevunja mkataba na klabu ya CD Tenerife ya Hispania kwa kutopata nafasi ya kutosha ya kucheza, badala yake Amunike amemuita mshambuliaji aliyetupiwa virago na Botswana Defence Force XI, Rashid Mandawa.

Usemi wa chanda chema huvikwa pete unaweza kutumika kueleza uamuzi wa benchi la ufundi la Taifa Stars kumpa nafasi mshambuliaji Adi Yussuf ambaye hivi karibuni alitia saini mkataba wa kujiunga na Blackpool inayoshiriki Ligi Daraja la Pili England.

Hata hivyo, hakukuwa na nafasi kwa nyota wa timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 'Serengeti Boys', Kelvin John kama ilivyo kwa kipa wa timu ya Taifa chini ya umri wa miaka 20, Claryo Boniface.

Ukiondoa watano hao, wengine ambao hawakujumuishwa ni Miraji Athumani, Fred Tangalu, Selemani Salula na David Mwantika.

Kikosi cha wachezaji 23 watakaoiwakilisha Taifa Stars ni makipa Aishi Manula (Simba), Metacha Mnata (Mbao) na Aron Kalambo (Prisons).

Mabeki: Hassan Kessy (Nkana FC), Gadiel Michael (Yanga), Mohammed Hussein 'Tshabalala (Simba), Kelvin Yondani (Yanga), Aggrey Morris (Azam) Vincent Philipo (Mbao) na Ally Mtoni 'Sonso' (Lipuli).

Viungo: Himid Mao (Petrojet), Feisal Salum 'Fei Toto' (Yanga), Yahya Zaydi (Ismailia), Mudathir Yahya (Azam), Frank Domayo (Azam), Farid Musa (Tenerife) na Erasto Nyoni (Simba).

Washambuliaji: Mbwana Samatta (Genk), John Bocco (Simba), Rashid Mandawa (Huru), Thomas Ulimwengu (JS Saoura), Saimon Msuva (Difaa El Jadida) na Adi Yussuf (Blackpool).