VIDEO: CCM yafuta kura za maoni, Dar yaongoza kwa rafu

Tuesday October 22 2019

Katibu mkuu wa CCM, Dk Ali Bashiru akizungumza

Katibu mkuu wa CCM, Dk Ali Bashiru akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni katibu wa itikadi na uenezi, Humphrey Polepole. Picha na Ericky Boniphace 

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally ameagiza kurudiwa kwa uchaguzi wa wagombea uongozi wa serikali za mitaa ndani ya chama hicho katika maeneo yaliyolalamikiwa nchi nzima kwamba yamekiuka kanuni za uchaguzi huo.

CCM ilifanya uteuzi huo wa ndani ili kupata wagombea kwa ajili ya uchaguzi uliopangwa kufanyika Novemba 24.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za makao makuu ya chama hicho Lumumba jijini Dar es Salaam jana, Dk Bashiru pia ametaka mkoa wa Dar es Salaam urudie kazi hiyo ili kuhakiki mchakato wa uchaguzi.

“Yapo maeneo hawakufuata kanuni, na katika baadhi ya maeneo hayo kumekuwa na mgongano kiasi cha wanachama kususa kupiga kura,” alisema.

Alitaja kasoro hizo kuwa ni pamoja na kubadilishwa kwa vituo vya kupigia kura na hivyo kuwachanganya wanachama.

“Kuna maeneo wasimamizi walichelewa na hasa Kinondoni ambako wapigakura walijitokeza kwa wingi. Kulikuwa na usimamizi mbovu na kuruhusu watu wasiohusika kupiga kura,” alisema Dk Bashiru.

Advertisement

Pia, alisema hakukuwa na uzingatiwaji wa jinsia na maeneo mengine siri za chama zimevuja, jambo alilosema lilisababisha taharuki isiyokuwa ya lazima.

Akitoa maagizo kutokana na mvurugiko huo, Dk Bashiru alitoa siku mbili za nyongeza ili kurejewa kwa uchaguzi huo, huku akitaka kusiwe na mchujo wa wagombea.

“Kuwepo na kuzingatiwa kwa kanuni za kupiga kura na wagombea wote wapigiwe kura bila kupitia hatua ya mchujo,” alisema Dk Bashiru.

“Baadhi ya maeneo kulikuwa na kupishana kwa muhtasari, kuna kutofautiana kwa maamuzi ya kata na ya wilaya. Maeneo hayo yote uchaguzi huo urudiwe na wakirudia, hakuna kuchukua fomu za mchujo, zile fomu na majina ya walioomba wote wapigiwe kura.

Kuhusu kuvujisha siri, alisema chama kina msemaji ambaye ni Humphrey Polepole na hivyo kupiga marufuku kwa wanachama wengine kutoa taarifa bila idhini yake.

Aliwataka wanachama kufuata katiba, sheria na kanuni za nchi na chama.

Advertisement