VIDEO: Dar waongeza vituo vya kuchukua sampuli za corona

VIDEO: Dar waongeza vituo vya kuchukua sampuli za corona

Dar es Salaam. Uongozi wa mkoa wa Dar es Salaam umeteua hospitali za Serikali na binafsi 25 ili kuchukua sampuli kutoka kwa washukiwa wenye virusi vya corona na kuzipeleka maabara kuu ya Taifa.

Pamoja na hospitali hizo, pia kuna vituo mbalimbali katika jiji hilo vilivyomo kwenye mpango huo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema jana kuwa vituo na hospitali hizo hazitatumika kupima sampuli, bali kukusanya ili kurahisisha wanaohisiwa kupata huduma ya vipimo kwa kuchukuliwa sampuli kwenye maeneo yao ya karibu kabla ya kuchanganyika na watu wengine.

“Nafahamu yeyote anayejisikia homa, mafua hulazimika kwenda kituo cha afya, zahanati au duka la dawa kununua dawa. Lakini ndugu zangu mfahamu uwezekano wa mtu mwenye dalili za corona na kuambukiza wengine ni mkubwa sana. “Nimeamua kuja na mbinu mbadala ya kutenga hospitali na vituo vya afya 25 vya mkoa wa Dar es Salaam zitakazotumika kwa mtu yeyote mwenye dalili ya homa kali na mafua hasa yule anayehisi kuwa na virusi vya corona,” alisema Makonda.

Katika maelezo yake Makonda, alisema hospitali za Serikali zikiwamo za rufaa na binafsi, zitakuwa katika wilaya za Ilala (8) Temeke (4), Kinondoni (6), Ubungo (4)na Kigamboni (3).

Alitaja vituo hivyo kwa wilaya ya Kinondoni ni pamoja na Hospitali ya Mwananyamala na pia vituo vya afya vya umma vya Magomeni, Mikoroshini na Msasani.

Pia hospitali binafsi za IST clinic iliyopo Masaki, hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni na Rabininsia, iliyopo Wazo Hill.

Vituo vya kuchukuliwa sampuli katika wilaya ya Ilala ni pamoja na hospitali za Amana, Buguruni, Mnazi mmoja, Muhimbili na Burhani.

Kuna hospitali tatu kwenye mpango huo kwa wilaya ya Ilala nazo ni Hindu Mandal, Agha Khan pamoja na Regency.

Kwa upande wa wilaya ya Temeke kuna vituo vinne katika hospitali za umma za Temeke, Mbagala Rangi Tatu na Yombo na katika hospitali binafsi ya TOHS.

Makonda alitaja vituo vya wilaya ya Ubungo kuwa ni pamoja na Sinza, Kimara na Mloganzila na hospitali binafsi ya Bochi.

Wilaya ya Kigamboni ina vituo vitatu ambavyo ni Vijibweni, Kigamboni na hospitali ya Aga Khan.

“Kila eneo utakalofika utakutana na wataalamu wetu waliofundishwa watakaokupokea na kukuhudumia na kukupima magonjwa mbalimbali. Pale wanapobaini hauna magonjwa yote hayo wao watakuwa na mamlaka ya kuwasiliana na maabara ya Taifa ili uchukuliwe sampuli na kupimwa kama umeathirika na corona,” alisema Makonda.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, lengo la kuteua hospitali na vituo hivyo ni kuwasaidia wananchi wanaohisi wanaumwa kwa ajili ya kupata huduma, ikiwa ni sehemu ya jitihada za mkoa kulinda wataalamu wa afya pamoja na wananchi ili kupunguza msusuru wa watu wanaotakiwa kwenda karantini.

Makonda alibainisha kuwa mkoa wa Dar es Salaam umejipanga kupunguza ueneaji wa ugonjwa kwa kuainisha vituo maalum vya wahisiwa wanaokidhi vigezo vya tafsiri ya ugonjwa huo, kwa kuchukuliwa sampuli kwa ajili ya vipimo vya maabara katika maabara kuu ya Taifa.

“Wahisiwa wote wa ugonjwa wamekuwa wakipimwa katika maabara kuu ya Taifa na majibu yao kupatikana kwa wakati.

“Changamoto mojawapo ambayo imekuwa ikijitokeza ni baadhi ya watu wenye dalili za ugonjwa huu kupita katika vituo kadhaa vya kutolea huduma za afya na hivyo kuchangamana au kukutana na watu kabla ya kugundulika kuwa na ugonjwa. Hali hii inaweza kuchangia kuongezeka kwa wagonjwa kwa kasi kubwa,” alisema Makonda.