VIDEO: Hakuna mahututi wa corona-Waziri

Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile amesema watu 17 waliokuwa na maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya corona, Covid-19 waliopo nchini, wanaendelea vizuri na hakuna aliyelazwa.

Dk Ndugulile pia amesema hakuna uwezekano wa Serikali kupiga marufuku watu kutoka nyumbani katika siku za karibuni, isipokuwa kama hali itabadilika kwa kuwa wamejipanga kukabiliana nao.

Pia amewataka wanaopona kujitokeza hadharani kueleza hali waliyopitia ili kutoa elimu kwa umma.

Tanzania imeripoti watu 20 waliopata maambukizi ya virusi vya corona hadi kufikia jana, lakini mmoja alipoteza maisha mwanzoni mwa wiki hii na wawili wamepona, akiwemo Mtanzania wa kwanza kutangazwa kuwa na maambukizi, Isabela Mwampamba.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi Digital jana, Ndugulile, ambaye alikuwa akirejea idadi ya watu 19 wenye maambukizi kabla ya kuongezeka mmoja juzi, alisema wote waliosalia baada ya mmoja kufariki na wengine wawili kupona, wanaweza kutoka na kutembea.

“Na hawa 16 ambao wamebaki, hakuna hata mmoja ambaye naweza kusema amelazwa, au ni mgonjwa ambaye yuko kitandani, yuko hoi, hayuko,” alisema Naibu Waziri Ndugulile.

“Kwa hiyo wote hawa tumewakarantini ili kuhakikisha kwamba hawawezi kuambukiza watu wengine. Lakini hakuna mtu ambaye tunaweza kusema yuko serious (katika hali mbaya), ambaye yuko kitandani amelazwa.

“Kwa hiyo, hii kwetu ni jambo jema kwa sababu lina mantiki yake nyingine. Ukiangalia taarifa kutoka kwa wenzetu, unaona kuna ongezeko kubwa la wagonjwa ndani ya hospitali. Sisi bado hiyo hali haijajitokeza. Hao 16 ni watu ambao wanaweza kutoka huko mtaani, wakatembea na ukakutana nao na wala usihisi kama ni mgonjwa.”

Hadi jana saa 1:30 jioni, ugonjwa huo ulioanzia jiji la Wuhan katika jimbo la Hubei nchini China, ulikuwa umeshaua zaidi ya watu 50,200 na kuambukiza zaidi ya watu 980,000 kote duniani, kwa mujibu wa takwimu za worldometer.com.

Alisema tangu kutangazwa kuwapo kwa mgonjwa wa kwanza Machi 16, Serikali imechukua hatua za kudhibiti maambukizi na kwamba hatua zilizochukuliwa kwa sasa zinajitosheleza.

“Huu ni ugonjwa unaosambaa kwa kasi, mtu mmoja ambaye ameathirika anaweza kusambaza kwa watu wasiopungua watatu. Ukiangalia nchi nyingine walianza na mgonjwa mmoja, wakaja watatu, tisa ikaenda mpaka mamia,” alisema.

“Sisi kwetu hizi wiki tatu tangu tumepata mgonjwa wa kwanza, kasi ya ukuaji ni ndogo. Maana yake ni nini? Hatua tunazochukua zinajitosheleza. Tuko katika hali nzuri ya udhibiti.”

Alisema ikitokea wiki mbili zijazo wagonjwa wameongezeka, Serikali itachukua hatua za ziada za kukabiliana nao.

Alisema Tanzania ina mifumo imara na bora ya ufuatiliaji wagonjwa, hali inayowavutia watu wengi kutoka mataifa ya nje ambao wanakuja nchini kujifunza.

Alisema katika kuthibitisha hilo hata yalipotokea magonjwa ya mlipuko kama Ebola na mengine, Tanzania haikupata maambukizi.

“Tulianza kujiandaa mapema, tulianzia ngazi ya utayari na sasa tunadhibiti. Tulichokifanya kama nchi ni kuhakikisha wataalamu wa afya wanapata mafunzo pamoja na kuwapo vifaa vya kutolea huduma.

“Pia kila halmashauri na mkoa ina maeneo ya kutibu wagonjwa, sehemu ya kuwatenga watu. Mikakati tunaendelea kuitoa kidogokidogo kadri idadi ya wagonjwa inavyoongezeka.”

Kwa kuwa ugonjwa huo haujapata dawa, watalaamu wanasema tiba yake hulenga ugonjwa ambao dalili zake zimejitokeza huku wakiziachia kinga za mwili zipambane na virusi vya corona.

Akizungumzia hatua zilizochukuliwa na baadhi ya nchi ikiwamo na kuzuia watu kutoka nje, Dk Ndugulile alisema Tanzania imekuwa na uangalifu katika kuchukua hatua za kudhibiti kulingana na ukuaji wa ugonjwa huo.

“Bado tuna mikakati mingi ndani ya mifuko yetu,” alisema.

“Tunaangalia hali inakwendaje. Kama tukiona sasa tunahitaji kudhibiti mikusanyiko, tutafanya. Kama tunataka kukizuia kitongoji fulani kutokana na maambukizi tutafanya. Hivyo kuna hatua tutaendelea kuzichukua.”

Alisema hadi sasa maambukizi yametokana na watu waliotoka nje au waliokutana na watu waliotoka nje, hivyo hatua za kupunguza mikusanyiko na kuhimiza watu kunawa mikono zinatosha.

“Endapo tutaanza kuona ongezeko la wagonjwa wa ndani; mtu ambaye alikuwa Tandale au Chanika, tukamuona anakuja na ugonjwa wa Covid na hana historia ya kusafiri, hajawahi kukutana na Mzungu wala Mchina au mtu yeyote kutoka nje ya nchi, sasa hiyo inahitaji hatua kwamba sasa tunalimit (tunapunguza) kabisa movement (matembezi).”

Lakini kwa sasa Serikali inaendelea kufanyia tathmini na endapo itaona kuna ongezeko kubwa “hizo hatua nyingine zitafuata”, alisema.

Alisema kuna nchi zimechukua hatua ambazo zimeathiri pia wananchi, hivyo ni muhimu kuhakikisha hatua zinazochukuliwa zinakuwa na manufaa kwa wananchi, lakini haziathiri ukuaji wa ugonjwa huo.

Pamoja na hayo, alitoa wito kwa watu waliopona ugonjwa huo kujitokeza na kuzungumza na umma, ili kutoa matumaini kwa wananchi.

“Serikali haijakataza watu waliopona kuzungumza, ila sisi hatutoi taarifa za mgonjwa,” alisema.

“Mimi kama mtalamu wa afya hilo sioni kama tatizo, ili watu wapate uhalisi kuwa niliugua, nilitengwa kwa siku 14 na sasa nimepona. Hapa tunataka kudhibitisha kwamba mtu anaweza kuugua ugonjwa huu na kupona maana kuna dhana imejenga mtaani kwamba mtu akiugua ni lazima afe.”

Pia alisema hatua hiyo itaondoa unyanyapaa katika jamii, ndio maana wanafanya maandalizi kwa wagonjwa wanaotoka ili jamii iwapokee.

Ndugulile alisema kulingana na takwimu za Shirika la afya duniani (WHO), asilimia 80 ya wagonjwa watapata mafua ya kawaida, asilimia 20 watapata homa hali, huku vifo vikiwa chini ya asilimia tatu.

“Sio ugonjwa unaoua sana, tunawahimiza watu waliotoka nchi zenye maambukizi kupima na kukaa karantini kwa siku 14,” alisema.

Alisema kwa hatua ya sasa hawahimizi watu kupima, bali wanaochukuliwa vipimo ni wale wenye dalili, alikuwa amesafiri nje ya nchi katika nchi zilizoathirika na ugonjwa huo au alikutana na mtu aliyetoka katika nchi hizo.

Kuhusu mgonjwa aliyefariki, Dk Ndugulile alisema wanafuatilia mnyororo wa watu aliokutana nao tangu alipoanza matibabu katika hospitali binafsi.

“Tunawafuatilia marafiki, aliyemsafirisha kwenda hospitali, aliyemhudumia na wengine wote, ili kuwatenga. Hii ni hatua muhimu kwa kuwa mtu mmoja anaweza kuambukiza hadi watu watatu,” alisema.

Akizungumzia hatua wanazochukua ili kubaini mgonjwa amepona, Dk Ndugulile alisema humchukua vipimo zaidi ya mara tatu kila baada ya muda ingawa hawajaweka siku maalumu.

Alisema watu wanatakiwa kukaa karantini ama ujitenga, ili ugonjwa huo usisambae.

“Mtu aliyewekwa karantini anaangaliwa hali yake, akianza kuonyesha dalili anachukuliwa vipimo. Mtu aliyejitenga tuanza kumpima joto la mwili na atakapoanza kuonyesha dalili humchukua vipimo,” alisema.

Alisema mtu mmoja mwenye maambukizi anaweza kuambukiza hata watu watatu.

Kuhusu watu wenye magonjwa mengine kuwa hatarini wanapopata ugonjwa huo, Naibu Waziri huyo alikiri suala hilo na kutoa rai kwa watu hao kuchukua tahadhari za zaidi.

“Watu wenye magonjwa mengine kama kisukari, magonjwa ya moyo, figo, kansa, watu wanaoishi na virusi vya ukimwi wapo hatarini zaidi ya kupoteza maisha, hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari za ziada pamoja na kutumia kwa usahihi dawa wanazotumia, ili watakapopata maambukizi wasipate homa kali,” alisema.

Pamoja na hayo, alisema kisayansi ugonjwa huo hauwezi kuambukizwa kwa njia ya ngono, ila akatoa tahadhari iwapo mmojawapo atapata maambukizi.