VIDEO: Hii ndio sura ya Serikali atakayoiunda Dr Mwinyi

VIDEO: Hii ndio sura ya Serikali atakayoiunda Dr Mwinyi

Muktasari:

  • Hussein Mwinyi ameapishwa kuwa Rais wa Zanzibar na katika hotuba yake ameahidi serikali itakayozingatia nidhamu na maadili ya viongozi na watumishi, utendaji kazi wenye viwango bora na kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kuimarisha huduma za jamii.

Dar es Salaam. Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi ameahidi kuunda serikali makini itakayozingatia nidhamu na maadili ya viongozi na watumishi, utendaji kazi wenye viwango bora na kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kuimarisha huduma za jamii.

Rais Mwinyi ametoa ahadi hiyo leo Novemba 2 wakati  wa hotuba yake kwa Wazanzibar, baada ya kuapishwa kuwa Rais wa nane wa visiwa hivyo, akichukua nafasi ya Rais Ali Mohamed Shein ambaye amemaliza muda wake wa miaka 10.

Amesema atashirikiana na viongozi atakaowateua katika kufanikisha mipango yake ya maendeleo pamoja na ilani ya uchaguzi ya CCM na ahadi mbalimbali ambazo amezitoa kwa wananchi wakati wa kampeni.  

“Ninachoahidi ni kuunda serikali makini itakayozingatia nidhamu na maadili ya viongozi na watumishi, utendaji kazi wenye viwango bora na kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kuimarisha huduma za jamii kwa kuzitumia vema rasilimali zetu kwa manufaa ya taifa letu,” alisema.

Rais huyo mpya amesema serikali atakayoiunda itaongoza kwa msingi wa haki, uwajibikaji, uwazi na usawa kwa wananchi wote bila kumbagua mtu yoyote kutokana na itikati yake, jinsia au eneo analotola.

Amewapongeza wagombea wenzake wa nafasi ya urais ambao wamekubali matokeo na kukubali uamuzi wa wananchi. Ameahidi kushirikiana nao katika kuwatumikia wananchi na kuijenga Zanzibar mpya.

“Naahidi, niko tayari kuyaendeleza maridhiano yaliyo katika Katiba yetu na kushirikana nanyi katika kuijenga Zanzibar mpya. Zanzibar ni kubwa na muhimu kuliko tofauti zetu,” amesema Dk Mwinyi.

Kiongozi huyo pia amewapongeza wananchi kwa kutumia haki yao ya kidemokrasia kwa kuchagua viongozi. Pia, amewapongeza kwa kudumisha amani katika kipindi chote cha uchaguzi.

“Uchaguzi sasa umekwisha, kazi iliyo mbele yetu ni kushirikiana kwa pamoja katika kuiletea maendeleo nchi yetu. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kushiriki katika maendeleo ya nchi yetu na kutambua kwamba mchango wake ni muhimu,” amesema.