VIDEO: Kubenea ajitoa, Lissu na Mwakagenda kuchuana

Muktasari:

Chadema yaweka hadharani orodha ya wagombea wa nafasi ta uenyekiti na makamu wenyeviti bara na visiwani. Tundu Lissu na Sophia Mwakagenda kuchuana katika nafasi ya umakamu wenyeviti bara

Dar es Salaam. Mbunge wa viti maalumu wa (Chadema) nchini Tanzania, Sophia Mwakagenda atachuana na mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu kuwania nafasi ya umakamu uenyekiti Bara.

Endapo wakiteuliwa  na baraza kuu la  chama kesho Jumanne Desemba 17, 2019 wawili hao wanatarajiwa kuchuana Desemba 18, 2019 katika mkutano mkuu wa chama utakaokuwa na ajenda ya kufanya uchaguzi wa kumpata mwenyekiti na makamu wenyeviti wa bara na visiwani.

Mkurugenzi wa Itifaki, Uenezi na Mawasiliano wa Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amewaambia wanahabari leo, Jumatatu Desemba 16, 2019 kuwa katika nafasi waliojitokeza kuomba ni Lissu, Sophia huku Saed Kubenea ambaye ametangaza kujitoa.

Amesema Kubenea ametangaza kujitoa kupitia barua yake alioandika na kusoma kwenye kikao cha kamati kuu akieleza  anaamini Lissu ndiye anayeweza nafasi hiyo.

Amesema baada ya Lissu na Sophia kupita kwenye usaili wa kamati watakwenda kujadiliwa na kuteuliwa na baraza kuu ili kuteuliwa.

Kwa mujibu wa Mrema, nafasi ya umakamu uenyekiti wa Zanzibar aliyejitokeza ni Said Issa Mohammed anayetetea nafasi hiyo kwa mara nyingine.

"Nafasi ya uenyekiti waliopita kwenye usaili ni Freeman Mbowe anayetetea na Cecil Mwambe, ambao kesho watajadiliwa na baraza kuu ili kuteuliwa," amesema Mrema.