VIDEO: Mabadiliko makubwa kileleni ACT Wazalendo

Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad (kushoto) na Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe wakipongezwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho kwa kuchaguliwa kukiongoza chama chao, wakati wa mkutano mkuu wa pili uliofanyika jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ericky Boniphace

Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo jana kimemaliza rasmi mchakato wa uchaguzi wa viongozi wake wa kitaifa uliowaweka madarakani wanachama wazoefu, huku kikipitisha mabadiliko 18 ya katiba.

Katika uchaguzi huo, wanasiasa wawili mashuhuri nchini, Maalim Seif Shariff Hamad na Zitto Kabwe, walichaguliwa kushika nyadhifa mbili za juu zaidi ndani ya chama hicho, ikiwa ni miezi michache baada ya kundi la waliokuwa wanachama wa CUF kuhamia ACT Wazalendo baada ya uamuzi wa mahakama uliotambua uenyekiti wa Profesa Ibrahim Lipumba.

Maalim Seif, ambaye amewahi kuwa Waziri Kiongozi na baadaye Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) na ambaye ni mwanasiasa mashuhuri zaidi wa visiwani Zanzibar, alishinda nafasi ya mwenyekiti kwa kupata kura 337 sawa na asilimia 93.35 ya kura zote.

Naye, Zitto, mbunge pekee wa ACT katika Bunge la Jamhuri ya Muungano, alishinda nafasi ya Kiongozi wa Chama (KC), kwa kupigiwa kura 276, sawa na asilimia 73.6 ya kura zote.

Mbunge huyo wa Kigoma Mjini alipambana na mjumbe wa zamani wa Baraza la Wawakilishi, Ismail Jussa Ladhu. Jussa alipata kura 91, sawa na asilimia 24 ya kura zote.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam jana, mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya chama hicho, Omar Said Shaabani alisema mchakato ulikwenda vizuri na wana furaha kwamba chama kimemaliza uchaguzi kikiwa kimoja.

Wajumbe wa mkutano huo mkuu wa pili, waliwachagua Dorothy Semu na Juma Duni Haji kuwa makamu wenyeviti wapya wa chama hicho kwa upande wa Bara na Visiwani.

Kabla ya kuchaguliwa nafasi hiyo, Dorothy alikuwa kaimu katibu mkuu, wakati Duni alikuwa naibu kiongozi wa chama hicho akimsaidia Zitto.

Halmashauri Kuu inatazamiwa kumteua katibu mkuu, nafasi inayowaniwa na makada wa chama hicho, Ado Shaibu na Joran Bashange.

Mbali na uchaguzi wa viongozi hao, ACT Wazalendo pia imefanya mabadiliko ya katiba baada ya Sheria ya Vyama vya Siasa kufanyiwa marekebisho na pia baada ya kupokea maoni ya wanachama na wafuasi wa chama hicho.

Mjumbe mmoja wa kamati ya sheria ya ACT Wazalendo, alisema katika mahojiano na Weyani TV kuwa mapendekezo yote 18 yaliyowasilishwa katika mkutano huo yalizingatiwa na kupitishwa.

Alisema mbali na mabadiliko yaliyotokana na mabadiliko ya sheria, pia walipokea maoni ya wanachama na wafuasi, ambayo yalipelekwa katika kamati yao, ikaandaliwa rasimu ambayo ilipelekwa Halmashauri Kuu na baadaye kupitishwa na mkutano mkuu.

Alitaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni nafasi ya bodi ya wadhamini na mfumo wa upigaji kura.

Ujio wa Maalim, wenzake ACT

Maalim Seif aliondoka CUF baada ya kushindwa katika kesi aliyofungua dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Mwanasheria Mkuu na Profesa Lipumba.

Katika kesi hiyo, Maalim Seif na wenzake walitaka Mahakama Kuu itengue barua ya Msajili ya kutambua uenyekiti wa Profesa Lipumba. Hiyo ilitokea baada ya mgogoro wa uenyekiti wa Profesa Lipumba kumfikia Msajili, ambaye alisema baada ya msomi huyo kuandika barua ya kujiuzulu nyadhifa zote mwaka 2015, hakuna kikao kilichoitishwa kuridhia uamuzi wake.

Profesa Lipumba alijiuzulu nyadhifa zake mwaka 2015 na kukaa nje hadi mwaka 2016 aliporejea na kuandika barua ya kubatilisha kujiuzulu kwake.

Akizungumzia uchaguzi huo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Muhidini Shangwe alisema amevutiwa na namna mchakato mzima wa uchaguzi ulivyoendeshwa.

“Tumeona midahalo ikirushwa mubashara na washindani wakitoa hoja zao. Hii michakato ya uchaguzi imekuwa na changamoto nyingi nchini kwetu na nilifurahi kwamba angalau tumeona uwazi kwenye uchaguzi wa ACT Wazalendo,” alisema mhadhiri huyo.

Kwa matokeo ya uchaguzi huu, ina maana chama hicho kitakuwa na viongozi wawili wa juu; Zitto na Maalim Seif.

“Wakati Zitto ni mwanasiasa kijana machachari na asiyeogopa kutoa maoni yake, Maalim ni mwanasiasa mzoefu, anayezungumza maneno yake kwa kupima na mwenye uwezo wa kufanya siasa za majukwaani na katika meza za mazungumzo,” alisema mhadhiri huyo.

“Waanzilishi wa ACT Wazalendo walikuwa ni wanasiasa ambao hawajawahi kuongoza nchi wala kufanya kazi serikalini, lakini kuingia rasmi katika uongozi kwa akina Maalim Seif kunamaanisha kwamba chama hiki sasa kitaongozwa na watu wenye maarifa na uzoefu wa kuongoza ndani na nje ya serikali.”

Mmoja wa wajumbe waliohudhuria Mkutano Mkuu wa ACT Wazalendo, alisema ACT Wazalendo sasa itaweza kuvutia hata wahafidhina wa CCM Zanzibar ambao wasingeweza kujiunga na CUF kwa sababu ya historia ya CCM na CUF ya Maalim Seif.

Mjumbe huyo, ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake, alisema uchaguzi huo pia unampa Zitto na ACT Wazalendo fursa ya kuondoa dhana kuwa chama hicho ni cha mtu mmoja au watu wa eneo moja la nchi kwa sababu sasa kitakuwa na viongozi wengi kutoka maeneo tofauti ya nchi.

Uchaguzi Mkuu Zanzibar 2020

Dk. Shangwe alisema uchaguzi wa viongozi umezindua rasmi siasa za Zanzibar kwa sababu umempa Maalim Seif chombo na mamlaka ya kukiongoza chama chake katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

“Mgogoro uliokuwepo ndani ya CUF uliweka ukungu na sintofahamu katika siasa za Zanzibar, lakini uchaguzi huu sasa utampa nafasi Maalim Seif na wanasiasa wa visiwani kujiandaa kwa uchaguzi huo kwa kutumia chama ambacho hakina makandokando ya siasa za nyuma za visiwa hivyo,” alisema..

“Ukweli kwamba sasa Maalim atakuwa na Zitto katika timu yake, maana yake ni kwamba amepata mtu ambaye ana ushawishi mkubwa ndani ya siasa za Tanzania na nje ya nchi.”

Dk Shangwe alisema CUF ilikuwa ikibebwa zaidi na Maalim kwa sababu waliokuwa viongozi wa chama hicho upande wa Bara; James Mapalala, Musobi Mageni na Ibrahim Lipumba hawakuwahi kuwa na kiwango cha ushawishi na umaarufu kama wa Zitto.

Katika mahojiano ya Mwananchi na baadhi ya wajumbe wa mkutano huo walionekana kufurahia sura mpya ya chama hicho wakisema wanaamini itawapa ushindi katika uchaguzi wa mwaka huu.