VIDEO: Maji ya ziwa Victoria yavunja rekodi

VIDEO: MAJI YA ZIWA VICTORIA YAVUNJA REKODI

Muktasari:

Kuna uwezekano wa rekodi hiyo kuvunjwa zaidi kutokana na taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa



Mwanza. Rekodi ya wastani wa kina cha maji kutoka usawa wa bahari ndani ya Ziwa Victoria iliyowekwa miaka 55 iliyopita imevunjwa mwaka huu baada ya kuongezeka.

Mei, 1965, WataalamU wa haidrolojia walirekodi kiwango cha juu cha wastani wa kina cha maji kutoka usawa wa bahari ndani ya Ziwa Victoria kuwa ni mita 1, 134.27.

Rekodi hiyo imedumu kwa miaka 55 hadi Machi 28, ilipovunjwa baada ya wastani wa kina cha maji kutoka usawa wa bahari ndani ya ziwa hilo linalochangiwa na nchi tatu za Afrika Mashariki za Tanzania, Kenya na Uganda kufikia mita 1, 134.47.

“Kuna uwezekano wa rekodi hiyo kuvunjwa zaidi kutokana na taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini kuonyesha kuwa bado mvua nyingi zinatarajiwa kunyesha Aprili hadi Mei, 2020,” alisema Ofisa Uhusiano wa Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB), Gerald Itimbula.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalum ofisini kwake jana, Itimbula alisema: “Kihaidrolojia ongezeko la maji ziwani ni jambo la neema kwa sababu tunahitaji mengi zaidi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi kuanzia kwenye kilimo, ufugaji, usafirishaji, uvuvi na viwandani.”

Hata hivyo, alisema ongezeko hilo linaweza kuwa na madhara katika baadhi ya masuala ya kijamii na kwa watu wanaofanya shughuli zao karibu au pembezoni mwa ziwa.

“Februari 8, tulihadharisha umma kwa umma kuwataka wote wenye shughuli za kibinadamu kama makazi, biashara na kilimo pembezoni mwa ziwa kuchukua tahadhari. Bado tunasisitiza hilo kwa sababu tunatarajia maji yataongezeka zaidi,” alisema Itimbula.

Bonde la Ziwa Victoria ndicho chombo chenye dhamana ya kufuatilia hali ya maji kwa kuangalia kiwango na ubora wa maji ndani ya Ziwa Victoria ambayo asilimia 80 ya maji yake yanatokana na mvua huku asilimia 20 ikitegemea vyanzo vingine vikiwemo mito na vijito vinayomwaga maji yake ziwani.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti juzi, wakazi wa eneo hilo, Sebastian Chibuye na Leah Jumanne walisema mara nyingi maji hayo huingia kwenye makazi yao wakati mawimbi makubwa yanapovuma ziwani.