VIDEO: Makonda aja na jambo jipya Dar

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akionyeshwa na Mhandisi wa Shirika la Nyumba la Taifa(NHC), Elisante Ulomi jinsi ujenzi unavyoendelea wa machinjio ya Kisasa Vingunguti jijini Dar es Salaam alipofanya ziara jana. Picha na Anthony Siame

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewaomba mawaziri wamvumilie kufanya ziara katika mkoa wake ili akamilishe maelekezo yaliyotolewa na Rais John Magufuli kuhusu miradi ya maendeleo, ingawa baadhi ya wasomi wamesema hatua hiyo si sahihi.

Wasomi hao wamesema Makonda ana uwezo wa kutekeleza miradi hiyo na kupokea maagizo kutoka kwa mawaziri watakaofanya ziara mkoani Dar es Salaam na wakamshauri aangalie jinsi ya kujipanga.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda amesema mkuu huyo wa mkoa anaweza kutekeleza majukumu yake yote bila kutoa sababu.

Mtazamo wa Dk Mbunda unafanana na wa mkurugenzi wa zamani wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo- Bisimba aliyehoji “avumiliwe wakati yupo kazini? Anachotakiwa ni kutoa mpango kazi wa utekelezaji majukumu yake badala ya kuomba mawaziri wamvumilie.”

Makonda alitoa ombi hilo jana ikiwa ni siku moja tangu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo kukagua miradi ya maendeleo mkoani Dar es Salaam na kumpa siku 14 kuhakikisha anaitisha kikao cha taasisi zinazovutana kutekeleza ujenzi soko la kisasa la Kisutu.

Taasisi hizo ni Manispaa ya Ilala, Ofisi ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads-Dar es Salaam) na Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) ambazo zimeshindwa kuafikiana katika ujenzi huo.

Jafo alitoa maagizo hayo juzi wakati akikagua ujenzi wa soko hilo, akisema “ndani ya wiki mbili (Makonda) aitishe kikao na manispaa ya Ilala, Tanroads Dar es Salaam na BRT kwa sababu yupo ndani ya ofisi yangu, nipate taarifa haraka.”

Mkataba wa ujenzi wa soko hilo ambao ulisainiwa Juni 28, 2018 ujenzi wake ulikuwa uanze Julai mwaka huo na meya wa manispaa hiyo kipindi hicho, Charles Kuyeko alisema ujenzi ungefanyika kwa miezi 18 kwa gharama ya Sh13.48 bilioni kutoka Serikali Kuu.

Kuyeko, ambaye Machi 23 alijiuzulu umeya na uanachama wa Chadema na kuhamia CCM, alisema kukamilika kwa soko hilo kungewanufaisha wafanyabiashara 1,500.

Alichokisema Makonda

Jana, baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa machinjio ya Vingunguti na kuridhishwa na hatua iliyofikiwa, Makonda alitoa ombi kwa mawaziri akisema kama itapendeza wamvumilie ndani ya mwezi unaoisha leo na Oktoba wasifanye ziara mkoani kwake. “Baada ya hapo waje wafanye ziara katika mkoa huu, wavumilie kidogo nikamilishe kufuatilia yale yaliyoelekezwa na mheshimiwa Rais na yale yaliyojiri katika mkutano uliofanyika Septemba 25 kati yangu na watendaji wa mkoa huu.

Makonda aliiagiza manispaa ya Ilala, kuanza usanifu wa kukarabati barabara ya urefu wa kilomita moja inayotoka maeneo ya Vingunguti mataa hadi eneo la machinjio.

Makonda pia alitembelea soko la kisasa la Kisutu na kuagiza ujenzi wake ufanyike usiku na mchana ili ukamilike kwa wakati.

Hayo yanajiri zikiwa zimepita siku kadhaa tangu Rais Magufuli kusema kuwa haridhishwi na kasi ya utekelezaji miradi Dar es Salaam na kuhoji kama mkoa huo una viongozi hasa miradi ya machinjio ya Vingunguti na ufukwe wa Coco.

Wasomi wazungumza

Akizungumzia ombi la mkuu huyo wa mkoa kwa mawaziri, Dk Mbunda alisema “hatakiwi kusema hivyo kwa sababu anaweza kupokea maagizo ya mawaziri na kazi ya kutekeleza miradi hiyo ikaendelea kama kawaida. Kiongozi lazima uwe mnyenyekevu kwa mwenzako aliyekuzidi cheo.”

Dk Mbunda anaungwa mkono na Dk Bisimba aliyesema, “mawaziri wapo kazini na yeye yupo kazini, ni vyema ‘akaji-fix’ na ratiba zake ili atekeleze majukumu yote na yale atakayopewa na viongozi hao badala ya kuomba wamvumilie.”

Mhadhiri msaidizi wa UDSM, Faraja Kristomus alitafsiri kauli ya Makonda kwa mtazamo tofauti “inawezekana amewaomba mawaziri wamvumilie wasifanye ziara kwanza ili akamilishe miradi hiyo. Kwa sababu mawaziri hawa wakifanya ziara wanarudisha mrejesho kwa Rais Magufuli. “Ameomba kuweka mambo sawa kuhakikisha miradi hii inakwenda vizuri.”

hasa baada ya Rais Magufuli kusema haridhishwi. Nadhani kawaomba wafanye ziara mikoa mingine ili wakija Dar es Salaam wakute mambo sawa,” alisema Kristomus.

Mradi ulipofikia

Mhandisi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), ambao ndio watekelezaji wa mradi wa machinjio ya Vingunguti, Elisante Ulomi alisema kwa sasa wwapo katika hatua ya ufukiaji na ushindiliaji wa udongo wa msingi kazi itakayofanyika siku moja na nusu.

“Baada ya hapo tutapanga mawe ya msingi, kisha kusuka nondo ambazo zitakuwa na kazi ya kuongeza uimara wa msingi huu. Ifikapo Novemba 20 tutakuwa tumeshapaua.

Meya wa Ilala, Omar Kumbilamoto alisema wameyapokea maagizo yaliyotolewa na Makonda na kuahidi kuwyafanyika kazi kupitia watendaji wa halmashauri hiyo, pamoja na baraza la madiwani.

Ujenzi wa machinwjio ya Vingunguti wenye thamani ya Sh12.47bilioni ukikamilika ng’ombe 1,000 na mbuzi 500 watakuwa wakichinjwa kila siku.