VIDEO: Mazrui aachiwa aibukia mkutano wa Maalim Seif

VIDEO: Mazrui aachiwa aibukia mkutano wa Maalim Seif

Muktasari:

Mazrui amedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana na polisi walisema wanafuatilia tukio hilo

Unguja. Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Nassor Ahmed Mazrui ameachiliwa huru baada ya kushikiliwa kwa zaidi ya saa tano na watu wasiojulikana waliodaiwa kumteka asubuhi ya leo Jumapili Oktoba 27.

Tukio hilo limetokea asubuhi eneo la Kikosi cha Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar ( JKU) Saateni wakati akitoka nyumbani kwake Mwera kwenda Makao Makuu ya ACT-Wazalendo yaliyopo Vuga.

Taarifa za kuchukuliwa kwa Mazrui zilianza kusambaa asubuhi kisha viongozi wakuu wa ACT-Wazalendo akiwemo Maalim Seif Sharif Hamad na Zitto Kabwe wakatoa matamko kwa nyakati tofauti wakitaka watu waliomchukua kiongozi huyo wamwachie huru.

Mapema, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Awadh Juma Haji akizungumza kwa simu na Mwananchi alithibitisha kuwapo kwa taarifa hizo, akisema jeshi hilo  linaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.

"Uchunguzi ukikamilika tutatoa taarifa zaidi. Kwa sasa siwezi kulielezea kwa urefu tukio hilo ila ni kweli tumepokea taarifa hizo tumeshaanza kuzifanyia kazi,” alisema Kamanda Haji.

Alivyoibuka

Majira ya saa 9 kasoro alasiri leo wakati mkutano wa kufunga kampeni za Maalim Seif unaofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, ghafla umati ulipigwa na butwaa baada ya kuonekana gari iliyombeba Mazrui ikiingia uwanjani hapo.

Tukio hilo lilitokea wakati, Mgombea mwenza wa Urais wa chama hicho, Profesa Omary Fakhii akizungumza na wananchi hao, ndipo kelele za zikaripuka na watu wakaruka uzio wa kamba kwa ajili ya kumuona Mazrui ambaye baada ya kushuka kwenye gari alikumbatiwa na Maalim Seif huku wafuasi wakimkaribisha.

Kwa mujibu wa Katibu wa itikadi, uenezi na mawasiliano kwa umma wa chama hicho, Salim Biman, Mazrui ambaye ni mwenyekiti wa timu ya ushindi wa kampeni za Maalim Seif atapata fursa ya kueleza tukio hilo baadaye.