VIDEO: Mchungaji Msigwa atoka jela

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa

Muktasari:

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa leo jioni Jumatano Machi 12, 2020 ametoka katika gereza la Segerea baada ya kulipiwa faini ya Sh40 milioni.

Dar es Salaam. Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa leo jioni Alhamisi Machi 12, 2020 ametoka katika gereza la Segerea baada ya kulipiwa faini ya Sh40 milioni.

Msigwa ametoka gerezani baada ya Chadema kusema kuwa wameshamlipia faini, baadaye Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa kueleza kuwa Rais Magufuli ametoa Sh38 milioni ili ndugu wa mbunge huyo waliochangishana Sh2 milioni, kuongezea na kumtoa jela.

Hata hivyo, mkurugenzi wa itikadi, uhusiano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema amesema, “sisi kama chama tumelipa Sh100 milioni ya watu watatu ambao ni Peter Msigwa, John Mnyika na Salum Mwalimu na tumewalipia kupitia benki tawi la Azikiwe.”

“Tumeshapeleka malipo mahakamani, tunasubiri risiti za mahakama. Kama kuna mwingine amemlipia Mchungaji  Msigwa hatuna ushahidi na uhakika nao, kama chama mahakama haijaturejeshea fedha za Msigwa kwamba kalipiwa mara mbili.”

Kuhusu mazingira ya Mchungaji Msigwa kuondoka  gerezani, Mrema amesema kilichoshangaza na msafara wa magari ya Serikali na katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kuelekea gereza la Segerea kwa ajili ya kumchukua mbunge huyo wa Iringa Mjini.

Mrema amedai Mchungaji Msigwa aliondoka na gari la wakili wa Chadema.

“Msigwa aliondoka leo jioni na mwanasheria wetu , hatuwezi kusema ameelekea wapi kwa sasa.”

Katika akaunti yake ya Twitter, Meya wa Manispaa ya Ubungo kupitia Chadema, Boniface Jacob aliandika, “baada ya mapambano makali na mchungaji Msigwa kugomea kupanda magari yao katika gereza la Segerea, Mchungaji Msigwa ametaka gari la wakili wa Chadema ndiyo liruhusiwe kuingia ndani kumchukua bila kurekodiwa na kamera zao.”

Wakati Mrema akieleza hayo, maelezo ya malipo ya Mchungaji Msigwa yaliwasilishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Gerson Msigwa aliyeambatana na Mchungaji Beneth Msigwa aliyesema  kuwa ni ndugu wa Rais Magufuli.

“Baada ya hukumu familia (ya Mchungaji Msigwa) walitafuta Sh2 milioni na kwenda kwa Rais Magufuli ambaye aliongeza Sh38 milioni wakaenda kulipa. Hapa wameleta risiti na wanaelekea gerezani kwa ajili ya kumtoa Mchungaji Msigwa,” amesema Gerson Msigwa.

Mbunge huyo wa Iringa Mjini  ni kati ya viongozi wanane wa Chadema ambao pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji Jumanne Machi 10, 2020 walihukumiwa kulipa faini ya Sh350 milioni au kwenda jela miezi mitano baada ya kutiwa hatiani kwa makosa 12 kati ya 13 yaliyokuwa yanawakabili.

Washtakiwa hao wakiongozwa na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe walilazimika kwenda jela baada ya kushindwa kukamilisha taratibu za kulipa faini hiyo waliyohukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Baada ya hukumu hiyo iliyosomwa  na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, Chadema walianza kuchangishana fedha kwa ajili ya kuwalipia faini viongozi wake hao.

Leo  wabunge wengine waliolipiwa faini na kutoka mapema asubuhi ni  Ester Bulaya (Bunda), Esther Matiko (Tarime Mjini) na Halima Mdee (Kawe).

Ambao bado wapo katika gereza la Segerea ni mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, John Heche (Tarime Vijijini),  John Mnyika (Kibamba) na naibu katibu mkuu wa chama hicho-Zanzibar, Salum Mwalimu.