VIDEO: Mmiliki wa baa Dar abanwa na Waziri Lugola, aishiwa nguvu

Muktasari:

Mmiliki wa  Baa ya Buscar La Vida ya Mbezi Beach aishia nguvu mbele ya Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola wakati akitoa maelezo kuhusu mwenendo wa shughuli za baa hiyo.

Dar es Salaam. Mmiliki wa baa ya Buscar la Vida Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, Celina Koka amejikuta akiishiwa nguvu ghafla baada ya kumaliza kutoa maelezo yake kwa Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola kuhusu mwenendo wa baa hiyo.

Lugola amefanya ziara leo Jumatatu Septemba 9, 2019 katika bar hiyo iliyopo eneo la Mbezi Beach wilayani Kinondoni.

Waziri huyo amefika katika baa hiyo yenye kumbi ya starehe baada ya kupokea malalamiko ya wananchi wa maeneo hayo wakiwemo majirani waliokuwa wakilalamika kupigiwa kelele na muziki unaopigwa katika eneo hilo.

Katika maelezo yake kwa Lugola, Celina amedai wamekuwa wakifanya kazi kwa shida katika eneo hilo sanjari na kufungiwa licha ya kufuata taratibu zote ikiwemo kwenda kwa wajumbe wa nyumba kumi kuhusu shughuli zao.

 “Hatutaki kuvunja sheria za nchi na siyo sisi tu tunaopiga muziki wapo wengi, kama ni operesheni iwe kote ili tuwe na amani. Lakini imekuwa ni kwangu tu hapa na nimeshafanya vikao vingi na majirani lakini baadhi hawafiki,” amesema Celina

“Hapa mheshimiwa kuna chuki binafsi kutoka kwa kina mama wenzangu ambao wamekuwa wakinisakama na baadhi yao walishadiriki kuniambia kuwa baa hii lazima iondoke katika eneo hili,” amesema

Hata hivyo, wakati akiendelea kuzungumza baadhi ya majirani walidai anachokizungumza siyo sahihi na kwamba baa hiyo imekuwa kero kwao kutokana na muziki mkubwa unaopigwa eneo hilo.

Baada ya kumaliza kuzungumza, Celina alijikuta akiishia nguvu mbele ya Lugola na wasaidizi wake waliamua kumshika na kumuondoa katika ya watu na kumweka pembeni.

Celina alikalishwa katika kiti na kuanza kupepewa huku akionekana kushika kichwa chake na kujipiga mikono kifuani  na alikuwa mwenye huzuni huku wasaidizi wake wakiangua kilio wakiamini kwamba baa hiyo inafungwa na Serikali.

Baadhi ya majirani wa eneo hilo wamedai kuwa malalamiko dhidi ya baa hiyo ni makubwa na anachokisema Celina ni uongo anajaribu kujitetea mbele ya Lugola.

“Hapa muziki unapigwa kuanzia Ijumaa tena ule wa live bendi na watu wanakaa zaidi ya mita 200 lakini wanalalamika. Tulishaandika barua kwa mkurugenzi kupinga eneo hili kubadilishwa matumizi, wao wana nyumba zao wanalala wanampumzika wakija hapa wanatuchagiza sisi tusilale mbona wanapora haki yetu ya msingi,” amesema Gasper Kigaraga

Baada ya maelezo hayo, Waziri Lugola aliwataka wamiliki wa baa, kumbi za starehe, taasisi za dini kwa maana ya makanisa na misikiti kufuata taratibu wakati wa kuendesha shughuli zao.

Naye Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc), Manchare Heche amemtaka Celina kupeleka nyaraka ofisini kwake ili kujiridhisha na uhalali wa uwepo wa baa hiyo ambayo ipo karibu shule.