VIDEO: Nancy Sumari ampa sylvia mbinu za kutamba miss world

Saturday November 30 2019

 Basila Mwanukuzi, mwananchi habari, gazeti la mwananchi, miss tanzania, Miss World

 

By Imani Makongoro na Nasra Abdallah, [email protected]

Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ikifanya vibaya kwenye mashindano ya urembo ya dunia, au Miss World.

Mbali ya kufanya vibaya, wakati fulani umaarufu wa mashindano hayo uliporomoka kabla ya kukufuliwa na Basila Mwanukuzi. Ukiachilia mbali mwaka 2005 wakati Nancy Sumari alifanikiwa kutwaa taji la mrembo wa dunia Afrika, hakuna mrembo mwingine kutoka Tanzania aliyefikia mafanikio hayo.

Gazeti hili lilifanya mahojiano maalumu na Nancy Sumari kuhusu shindano hilo ili malkia wa sasa, Sylvia Sebastian aweze kufanya vizuri katika mashindano ya dunia yatakayofanyika Desemba 4, 2019 jijini London, Uingereza na kuwatoa tena kimasomaso Watanzania.

Wakati wengi hudhani kuwa mwonekano ndio huchangia mshidndani kufanya vizuri katika mashindano ya dunia, Nancy ana mawazo tofauti.

“Urembo pekee si kigezo cha kukusaidia kushinda taji la dunia, kuna sifa kuu tatu za ziada ili kutwaa taji hilo,” anasema Nancy.

Nancy, aliyetwaa taji la Miss World Africa katika mashindano yaliyofanyika Sanya nchini China, anasema bila ubunifu ni vigumu kutwaa taji hilo ambalo linawania na warembo zaidi ya 300 kutoka kila pande ya dunia, kila mwaka.

Advertisement

“Sitaki kusema nini kilinifanya nishinde, lakini nashauri ukiwa kule kikubwa unachopaswa kufanya ni kuhakikisha unapata marafiki wengi, ikiwezekana washiriki wote wawe rafiki zako,” anasema.

Anasema njia hiyo huwafanya washiriki wengine kuwa rahisi kukupigia kura katika kipengele cha warembo kupigiana kura, hivyo hukuongezea nafasi ya kufanya vizuri zaidi,” anasema.

“Kingine ni kuwa mbunifu, unaweza kuwa na vazi maalumu la asili ambalo litakufanya uwe wa tofauti na kukutambulisha zaidi. Si lazima liwe la gharama kubwa, lakini libuni ili likutambulishe kama Mtanzania.

“Hiyo itawafanya washiriki wenzako kukuangalia na kukuzungumzia jambo litakalokufanya usisahaulike.

“Jambo muhimu kabisa ni kwenda kushiriki mashindano ya dunia, nikimaanisha usiwaze kushinda hadi ukasahau kushiriki. Shiriki kwanza kwa kuhakikisha unakuwa gumzo, unafanya kila jambo kwa ustadi kuliko wengine, una marafiki na unavaa vizuri, ndiyo ufikirie kushinda.”


Advertisement