VIDEO: Ndugai amvaa Lissu malipo ya mshahara

VIDEO: MAPYA YAIBUKA SPIKA NDUGAI NA TUNDU LISSU, SPIKA AITWA MUONGO

Dodoma. Spika wa Bunge Job Ndugai amesema aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amelipwa mishahara yake yote ukiwamo wa Juni 2019 ambao anadai hajalipwa.

“Mishahara yote zaidi ya Sh200 milioni amelipwa, anadai wapi? Wakati mwingine mtu awe na shukrani, posho mbalimbali zaidi ya Sh360 milioni amelipwa.

“Badala ya kunituhumu tuhumu. Kwa ujumla amelipwa zaidi ya Sh 500 milioni kwa kipindi alichokuwa Ubelgiji,” alisema Ndugai jana jioni mara baada ya Bunge kupitisha bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka 2020/2021.

Mbali na madai hayo, Spika alilitangazia Bunge kuwa Lissu vilevile alikuwa na madeni ya Sh70milioni aliyokopa maeneo mbalimbali kupitia Bunge na kumtaka arejeshe fedha hizo.

“Si vyema kuweka mambo ya mtu hadharani lakini ninalazimika kutokana na yeye kujitokeza kwenye mitandao,” alisema Ndugai.

Hata hivyo, alisema kama ataendelea wataenda mbali zaidi na kuhoji jinsi alivyotumia fedha za wananchi, mishahara ya dereva wake na mafuta ya kumpeleka jimboni wakati akijua anazitumia isivyo halali kwa sababu yupo nje ya nchi, jambo ambalo litamletea shida kwa kutakiwa kuzirudisha.

Hivi karibuni Lissu alinukuliwa akilalamika kutolipwa baadhi ya mishahara yake.

Aidha, Ndugai aliahidi kuweka wazi madeni na madai ya wabunge wote ifikapo Juni 30, mwaka huu huku akisema walio wengi kiinua mgongo chao kitakuwa kidogo.

Alisema hadi kufikia Juni 30, mwaka huu kila kitu kitawekwa hadharani vizuri kimahesabu.

“Madeni ni mengi sana, kila mmoja apige hesabu madai aliyonayo na madeni, kuwa na madeni makubwa ni kukosa sifa ya uongozi. Msiangalie bajeti ya Waziri Mpango na kuikosoa wakati ukiangalia mtu ameshindwa bajeti yake tena kwa mbali,” alisema.