VIDEO: Ndugai asema Tanzania haitajikinga na corona kwa kuiga nchi nyingine

VIDEO: Ndugai asema Tanzania haitajikinga na corona kwa kuiga nchi nyingine

Muktasari:

Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema Serikali ya Tanzania haiwezi kuchukua tahadhari ya kuzuia kuienea kwa virusi vya corona kama yanavyofanya baadhi ya mataifa duniani.

Dodoma. Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema Serikali ya Tanzania haiwezi kuchukua tahadhari ya kuzuia kuienea kwa virusi vya corona kama yanavyofanya baadhi ya mataifa duniani.

Amesema baadhi ya taratibu zinazotumika katika mataifa hayo, ikiwemo wananchi wanaokutwa mtaani kuchapwa viboko wakitakiwa kukaa ndani ni ngumu.

Akizungumza bungeni mjini Dodoma leo Jumanne Machi 31, 2020, Ndugai amesema, “tukumbuke  hatuwezi kuchukua vipimo vya Wazungu na kuvileta  hapa kama vilivyo ni ngumu sana tutatua watu wetu.”

“Lazima tuangalie mazingira yetu ya Tanzania na kuchukua hatua kutokana na mazingira hayo, kama ambavyo Bunge tumeangalia mazingira yetu na kuona tunafanyaje kazi na kuja na utaratibu huu.”

Amesema katika maeneo yenye masoko wanatakiwa kuchukua hatua kadhaa kama kuweka maji ya kunawa na sabuni, kutokaa karibu ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.

“Tuchukue hatua mbalimbali kuhakikisha tunapunguza misongamano kwa kadri inavyowezekana.”

“Kuna nchi polisi wanapiga watu viboko ikilazimika huko Serikali itafanya lakini hatuishauri kwa sasa, tunajaribu kuelimisha zaidi, kutoa wito na kumuomba Mungu atuepushe na janga hili ambalo limezitikisa nchi zenye uchumi mkubwa,” amesema Ndugai ambaye pia ni mbunge wa Kongwa mkoani Dodoma.