VIDEO: Ni vilio, vicheko hukumu mauaji ya RPC Barlow

Muktasari:

“Ilikuwa huzuni na furaha”. Ndivyo unavyoweza kusema ukitaka kuelezea hali iliyowakuta ndugu, jamaa na marafiki wa washtakiwa saba katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza nchini Tanzania, Liberatus Barlow.

Mwanza. “Ilikuwa huzuni na furaha”. Ndivyo unavyoweza kusema ukitaka kuelezea hali iliyowakuta ndugu, jamaa na marafiki wa washtakiwa saba katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza nchini Tanzania, Liberatus Barlow.

Wakati ndugu wa washtakiwa wanne waliotiwa hatiani na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa wakiangua vilio, ndugu wa washtakiwa watatu walioachiwa huru baada kubainika kutokuwa na makosa  walitokwa na machozi ya furaha.

Hali hiyo imejitokeza leo Jumanne Novemba 12, 2019 baada ya Jaji Sirialus Matupa kusoma hukumu ya kesi hiyo ya mauaji namba 192/2014 na kuwatia hatiani washtakiwa wanne.

Barlow aliuawa eneo la Kitangiri Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza  Oktoba 13, 2012.

Waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa ni Peter Muganyizi, Magige Mwita, Abdallah Petro na Abdulrahaman Ismail.

Wakati ndugu wa washtakiwa hao wanne wakiangua vilio kwa uchungu ndugu wa  Chacha Mwita, Buganizi Edward na Bhoke Marwa wao walilia kwa furaha baada ya ndugu zao kuachiwa huru baada ya kubainika kutohusika na mauaji hayo.

Licha ya kuwepo ukimya na utulivu wakati wa hukumu hiyo ikisomwa, polisi waliimarisha ulinzi ndani na nje ya Mahakama kabla na baada ya hukumu kusomwa.