VIDEO: Rubani wa ndege aliyerejesha mwili wa Nyerere asimulia maajabu ya safari

Friday October 11 2019

By Cledo Michael, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. “Rubani Ridhiwani Maimuni, aliyeendesha ndege iliyobeba mwili wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alishuhudia maajabu wakati wa safari hiyo ya kutoka London, Uingereza.

“Kila anga unayopita, japo ilikuwa usiku, unapewa salamu za pole,” alisema Maimuni akikumbuka safari hiyo wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi kuhusu Miaka 20 ya kumbukumbu za kifo cha Mwalimu Nyerere.

“Tukitoa taarifa tu, tunaambiwa clear to pass (mnaruhusiwa kupita). Poleni sana.”

Maimuni alikuwa akiendesha ndege aina ya Boeing 737-300 ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATC) iliyobeba mwili wa Mwalimu Nyerere na kuuleta nchini.

Kabla ya kwenda kuchukua mwili huo mwaka 1999, Serikali ya Uingereza ilikuwa tayari kutoa ndege ya Royal Airforce, hali kadhalika serikali ya Afrika Kusini.

Hata hivyo, wafanyakazi wa ATC waliomba kuufuata mwili wa Baba wa Taifa kwa kutumia ndege hiyo iliyokuwa na rangi za bluu, kijani, nyeusi na manjano za bendera ya Taifa ili kuithibitishia dunia kwamba Watanzania wanaendelea kumheshimu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

Advertisement

Kamati iliyoufuata mwili wa Mwalimu Nyerere iliongozwa na Waziri Mkuu Frederick Sumaye na jopo la marubani wakiongozwa na Kapteni Anderson Wililo na Kapteni Lessane (marehemu).

Kundi la ATC lililokwenda Uingereza pia lilijumuisha, wahandisi na wahudumu wa ndani wa Tanzania. Kutoka London ndege hiyo ilitua Cairo, Misri kabla ya kuingia Dar es Salaam.

Marubani walihakikisha ndege inaingia Dar es Salaam kwa wakati uliopangwa saa 3:15 asubuhi na walipokewa na umati mkubwa wa watu ukiongozwa na Rais Benjamin Mkapa.

“Mwili tuliuweka ndani ya ndege, tulitoa seats (viti) nne na sio kwenye cargo (mizigo) na saa 3:00 asubuhi tukaufikisha mwili hapa Tanzania kama tulivyoelekezwa,” anasema Maimuni.

“Ilikuwa ni kazi nzito sana. Kwenye moyo una majonzi, lakini pia unatetemeka kwa sababu umebeba mwili wa mtu mkubwa,” alisema rubani huyo.

Anasema safari hiyo kwake ni historia ambayo hawezi kuisahau kwani ilikuwa ni ya aina yake tofauti kabisa na nyingine ambazo aliwahi kuzifanya nje ya nchi.

Anasema ni safari ambayo ilikuwa ‘monitored’ (inafuatiliwa) kwa ajili ya masuala ya kiusalama hivyo ilihitaji umakini wa hali ya juu.

Maimuni mwenye umri wa miaka 65 sasa na ambaye anaishi Oysterbay jijini Dar es Salaam anasema mbali na kuwa rubani wa ATC, pia alikuwa mwanajeshi wa Jeshi la Wananchi (JWTZ).

Safari ya Mwalimu

Anasema safari hiyo ilikuwa ni ya aina yake kutokana na heshima ambayo Mwalimu alijipatia ulimwenguni.

Kimsingi heshima hiyo ilitokana na juhudi zake za kupigania uhuru na kuwaunganisha Waafrika kwa kushirikiana na waasisi wengine wa bara hili.

Maimuni anasema kwamba yeye kama rubani wakati ule alikuwa na majonzi na furaha kwa wakati mmoja. Anasema ilikuwa ni heshima kubwa kusafiri angani na mwili wa Baba wa Taifa na kwamba hata katika anga zote ambazo ndege hiyo ilipita kila nchi husika zilikuwa zikituma salamu za pole kwa Watanzania kutokana na msiba huo mkubwa.

Aichambua ATCL

Akiizungumzia ATCL ambayo ilitokana na mabadiliko ya mwaka 2002 yaliyoibadili ATC na kuwa ATCL, Maimuni anasema shirika la ATC lilikuwa halijiendeshi kibiashara na ndiyo moja ya sababu ya kuanguka kwa shirika hilo lililoanzishwa Machi, 1977.

Anaeleza kuwa moja ya ndoto ya Mwalimu Nyerere ilikuwa ni kuona Tanzania inajiimarisha katika usafiri wa anga, lakini ndoto hiyo haikuzaa matunda kutokana na kujiendesha kama shirika la umma.

Baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, usafiri wa anga kwa kiasi kikubwa ulikuwa mikononi mwa Kenya, wakati Tanzania yenyewe ilibaki na usafiri wa reli.

Kwa maana nyingine, Kenya, ambayo ilikuwa imeanzisha shirika lake la ndege la Kenya Airways, ndiyo iliyokuwa ikitawala usafiri wa anga wakati huo.

Anasema katika miaka hiyo ya enzi za Mwalimu hasa kati ya mwaka 1980 na 1981 ndege za ATC zilifanya safari nyingi za kitaifa na kimataifa kwa kutumia ndege zake ambazo nyingine ililazimika kuzikodi kwa ajili ya kwenda nchi mbalimbali kama Ugiriki, Madagascar, India, Italia na Misri.

Anaishauri ATCL kutumia fursa zilizopo hivi sasa katika kujiendeleza huku akisifu hatua ya Rais John Magufuli kulifufua shirika hilo na kwamba zipo fursa nyingi ambazo zikitumika ipasavyo, zitaongeza ushindani.

“Wapo wastaafu waliokuwa kwenye vitengo mbalimbali wakati ule, ni muhimu wakawatumia hao kwa ajili ya kupata uzoefu. Pia, wazitumie vizuri safari zilizopo kwa ajili ya kupata watalii wengi zaidi,” alisema.

Anashauri kuwa ni vema shirika likajiendesha kibiashara na viongozi kuzingatia weledi ili liweze kushindana katika soko la kimataifa.

Alivyoupata urubani

Anasema haikuwa kazi rahisi kwake kuwa rubani kwa kipindi kile kwa kuwa nafasi za kusomea urubani zilikuwa chache na ililazimu kwenda kusomea nje ya nchi.

Bahati hii ilimkuta wakati akiitumikia JWTZ kama ofisa kadeti.

“Nimeingia jeshini mwaka 1972, nikaenda mafunzo ya urubani mwaka 1974 nchini Canada nikiwa ni mwanajeshi wa kawaida,” anasema.

Haikuishia hapo. Anasema aliporudi nchini mwaka 1976 alijiunga katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Monduli na kutunukiwa cheo cha Luteni Usu na Mwalimu Nyerere.

Anasema wakati Jumuiya ya Afrika Mashariki inavunjika mwaka 1977 alipata nafasi ya kuwa rubani wa ATC kutokana na uzoefu aliokuwa nao kutoka vyuo mbalimbali duniani.

Anafafanua kuwa baada ya jumuiya hiyo kuvunjika kulikuwa na mahitaji ya marubani ili kulitengeneza shirika la ATC ambalo lilianzishwa kutokana na kuvunjika kwa Shirika la Ndege la Afrika Mashariki (EAA).

EAA ilimilikiwa kwa pamoja na nchi za Kenya, Tanzania na Uganda na hivyo kuvunjika kwake kulikuwa na athari kwa Tanzania.

 

Advertisement