VIDEO: Sumaye aacha fumbo

Muktasari:

Wakati ofisi yake ilipotuma mwaliko kwa waandishi wa habari juzi kuhusu mkutano wake wa leo, ubashiri ulikuwa mmoja tu; waziri huyo mkuu wa zamani anarejea CCM kama makada wengine waliokihama chama hicho tawala mwaka 2015, likiongozwa na mtendaji mwingine mkuu wa Serikali wa zamani, Edward Lowassa.


Dar es Salaam. Dakika 30 zilimtosha Frederick Sumaye kuzungumzia safari yake ya kisiasa akiwa Chadema na uamuzi wa kung’oka, lakini ameacha fumbo nyuma yake.

Wakati ofisi yake ilipotuma mwaliko kwa waandishi wa habari juzi kuhusu mkutano wake wa leo, ubashiri ulikuwa mmoja tu; waziri huyo mkuu wa zamani anarejea CCM kama makada wengine waliokihama chama hicho tawala mwaka 2015, likiongozwa na mtendaji mwingine mkuu wa Serikali wa zamani, Edward Lowassa.

Lakini wakati anamaliza mkutano wake, hakuna aliyejua Sumaye anaelekea wapi baada ya kusema ataendelea kubakia kwenye siasa na yuko tayari kushirikiana na chama chochote.

Mazingira ya mkutano wake na waandishi wa habari, mtindo wa kujipa mmuda kabla ya kutangaza chama anachoenda kama alivyofanya mwaka 2015 na ulinzi wa askari wenye sare na mambo mengine, yanaweza kuwa yameacha fumbo zaidi kuhusu mustakabali wa waziri mkuu huyo wa zamani aliyeng’ara katika kampeni za mwaka 2015.

Na mwaliko wake kwa waandishi ulitumia barua iliyokuwa na nembo ya Adamu na Hawa ya Serikali, lakini akatumia nafasi hiyo kuomba radhi kwa kasoro hiyo iliyoibua ubashiri kuwa angetangaza kurejea chama tawala.

Sumaye aliutumia mkutano wa jana kuelekeza shutuma kwa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akisema baada ya kutafakari kwa kina na kuona walioshiriki kumuangusha ni wajumbe wa Kamati Kuu, “nimelazimika kwa kulazimishwa kujiondoa Chadema kutokea leo hii na sijiungi na chama chochote cha siasa”.

“Niko huru kutumika na chama chochote ikiwa ni pamoja na Chadema kwa kutoa ushauri nakadhalika,” alisema Sumaye akisisitiza msimamo wake wakati akijiunga upinzani mwaka 2015 kuwa ataendelea kuimarisha upinzani.

“Najua katika kujikosha yatakuwepo maneno kama kupewa fedha na CCM au ACT- Wazalendo na kadhalika. Kama nilipokuja Chadema mlinipa fedha, basi na sasa nitakuwa nimepewa sijui na nani.”

Sumaye alisema wapo watakaoumizwa na uamuzi wake, lakini akasema umechangiwa na viongozi wa Kanda ya Pwani akitumia maneno ya Biblia, “rushwa huwapofua macho hao wanaona na kuyapotoa maneno ya wenye haki”.

Mbowe hakutaka kujibu tuhuma dhidi yake alipohojiwa na Mwananchi jana zaidi ya kusema wakati ukifika atafanya hivyo.

“Mimi ni mwanasiasa sitaacha siasa,” alisema Sumaye ambaye alikuwa mmoja wa wanachama wa Chadema aliyejitosa kuwania uenyekiti wa chama hicho katika uchaguzi utakaofanyika baadaye mwezi huu.

Ujumbe kwa Mbowe

Lakini Sumaye alisema waliomtendea mabaya katika uchaguzi wa kanda walidhani wanamkomoa, “lakini wamekijengea chama mazingira ya ovyo na ya aibu”.

“Mbowe najua utakuwa mwenyekiti wetu wa chama, hilo kundi lako linalojidai ndiyo ‘cabinet’ (baraza) yako ya ndani usipoliangalia litakuvunjia chama,” alisema

Akisoma taarifa yake kwa umakini mkubwa, Sumaye alisema pamoja na yote aliyotendewa aliamua kuchukua fomu, kuijaza na kuilipia Sh1 milioni, lakini baada ya kufanya uchunguzi ameona si busara kuendelea na safari hiyo.

‘Sumu haionjwi kwa ulimi’

“Inabidi leo nitangaze kuwa hiyo safari ya kugombea uenyekiti ngazi ya taifa naisitisha rasmi kwa usalama wangu, usalama wa wanachama na wa chama chenyewe,” alisema.

“Kwa bahati nzuri alipokuwa Arusha kwenye mkutano wa kanda (Jumamosi iliyopita Novemba 29), Mbowe alishatutahadharisha kuwa sumu haionjwi kwa ulimi.”

Sumaye alisema uchaguzi wa kanda na wa taifa utakaofanyika Desemba 18 umeacha majeraha mengi ambayo si ya kushindwa kwenye uchaguzi bali ya mgawanyiko ndani ya chama kwa sababu walikuwa wanachaguana kwa kutegemea kundi la nani.

“Kwa wale waliokuwa Team Mbowe, kulikuwa na nguvu kubwa kutoka nje ya kanda zilizotumika na ambao siyo Team Mbowe waliumizwa sana. Hiyo hali haijengi umoja na mshikamano katika chama,” alisema.

Shutuma kwa Mbowe

Sumaye alisema hakuwa na nia ya kugombea uenyekiti wa kanda, lakini akisema kuna kundi la wanachama waliokwenda kumshawishi agombee tena na ndio waliomchu kulia fomu, akaijaza na kuirejesha, jambo ambalo alisema lilimfurahisha kila mmoja.

“Nongwa ilikuja baada ya mimi kuamua kuchukua fomu ya kugombea kiti cha taifa. Pamoja ni haki yangu kwa katiba ya chama chetu, lakini nilikuwa na lengo la kuondoa hisia ambayo imejengeka sana katika jamii ndani ya Chadema hakuna demokrasia ya kweli,” alisema Sumaye aliyekuwa Waziri Mkuu kuanzia mwaka 1995 hadi 2005.

“Lakini la pili, nafasi ya mwenyekiti taifa ni ya Mbowe tu na haisogelewi na mtu yeyote. Mimi binafsi sikuamini hisia hizi kuwa ni za kweli ndiyo maana niliona haya yasipofutika yanatuchafulia jina la chama chetu, kumbe mimi ndiyo nilikuwa nimekosea sana kufikiri hivyo.

“Pamoja na nia hiyo njema, badala ya busara kutumika hata kama tungetaka kumlinda Mbowe wetu, njia za ovyo ndizo zilitumika”.

Pia alikuwa na ushauri kwa Mbowe.

“Ndugu yangu Mbowe najua utakuwa mwenyekiti wa chama, tafadhali uunganishe hayo makundi maana kwa jinsi ninavyowajua baadhi yao watawasumbua sana wale wengine.

“Bado natamani kuona chama cha upinzani kinachopishana uongozi na CCM kama ilivyokuwa kwenye nchi za wenzetu walioendelea. Lakini kwa hali hii, safari bado ndefu lakini tujitathimini kihalisia na kufanya marekebisho ya kasoro hizi na nyingine, safari inaweza kuwa fupi.”

Meya wa Ubungo, Boniface Jacob, ambaye ni mmoja wa watu wanaosema walimpia Sumaye fedha za kuchukulia fomu, alisema, “kuondoka kwa Sumaye kumenishtua lakini hakutaturudisha nyuma.

“(Kuondoka mkwa Sumaye) Kutaongeza usiri katika vikao vyetu na ile Chadema iliyokuwa inaulizwa kuwa imerudi nyuma, sasa utaiona inasonga mbele,” alisema.

“Sumaye alipaswa kusema ukweli kwa nini ameondoka si kweli kwamba ni kwa sababu kugombea nafasi ya mwenyekiti. Chama kilikuwa na mapenzi sana na yeye na ndiyo maana kilimpitisha peke yake kuwa mgombea wa nafasi ya mwenyekiti Kanda ya Pwani.”

Katika mkutano wa jana, maofisa wa polisi na askari wa kawaida wenye sare walikuwepo kwenye jengo la LAPF Kijitonyama kuhakikisha ulinzi kwa mtendaji huyo mkuu wa zamani wa Serikali, tofauti na mikutano yake mingine.

Katika mkutano huo pia alikuwepo katibu wa Kanda ya Pwani, Mabina ambaye baadaye alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo.

“(Haya) Ymetokea ndani ya eneo langu la kazi na kwa maana hiyo leo Jumatano nimewasilisha barua ya kujiuzulu nafasi yangu. Nitabaki kuwa mwanachama mwaminifu wa chama chetu,” alisema.