VIDEO: Wanawake watajwa chachu ya maendeleo nchi za SADC

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa baraza la biashara nchi za SADC, Charity Mwiya amesema  kuwawekea mazingira wezeshi wanawake kibiashara ni fursa muhimu kuweza kufikia malengo ikiwemo kukuza ajira  katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika(SADC).

Dar es Salaam. Kuwawekea mazingira wezeshi wanawake kibiashara imetajwa kuwa fursa muhimu kuweza kufikia malengo ikiwemo kukuza ajira  katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika(SADC).

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Agosti 5, 2019 na Mwenyekiti wa baraza la biashara nchi za SADC, Charity Mwiya kutoka nchini Namibia alipokuwa akiwasilisha mada katika uzinduzi wa maonyesho ya bidhaa katika wiki ya viwanda kwa nchi 16 wanachama wa SADC, Dar es Salaam nchini Tanzania

Mwiya amesema wanawake wengi ndiyo wapo kwenye biashara na ujasiriamali hivyo mazingira wezeshi yanafaa kuwekwa ili nchi hizo zifikie malengo.

"Tunahitaji mazingira wezeshi kwa ajili ya maendeleo ya kibiashara na kukuza ajira katika nchi za SADC, mimi ni mwanamke wa kwanza kuwa mwenyekiti wa kamati hii hatuwezi kuzungumzia biashara bila kumtaja mwanamke," amesema

Pia amesema SADC haiwezi kuzungumzia umoja ikiwa sekta zote hazijaungana.

"Mfano mzuri Tanzania mliweza  kushirikiana na sekta binafsi katika biashara, lakini pia nishukuru baraza la mawaziri la SADC kwa kuweka programu zinazohusiana na uanzishwaji wa biashara.”

"Jitihada za pamoja za umma na sekta binafsi zinazoweza kutoa rasilimali na wakati uleule tunaweza kuwa na ajira kwa vijana wetu. Nishukuru Serikali ya Tanzania kutambua baraza la SADC," amesema Mwiya.

Kauli mbiu ya maonyesho ya bidhaa katika wiki ya viwanda kwa nchi 16 iliyoanza leo Agosti 5 hadi 8, 2019 ya wanachama wa SADC ni Mazingira bora kwa maendeleo endelevu na jumuishi  ya viwanda, kukuza biashara kikanda na ajira.