VIDEO: Yanga, Simba ni hesabu kali

Muktasari:

Yanga inaikaribisha Simba katika mchezo ambao ikishinda inaweza kurudi kileleni mwa msimamo wa ligi.

Dar es Salaam. Baada ya kuahirishwa kutoka Oktoba 18, hatimaye lweo mchezo wa kwanza wa Watani wa Jadi unafanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Yanga inashuka uwanjani ikiwa mwenyeji wa mchezo huo, ikijivunia kutopotweza mchezo wowote hadi sasa, ikiwa imecheza mechi tisa, ikipata sare mbili na kushinda saba.

Simba, ambao ndio mabingwa watetezi, inashuka uwanjani ikiwa na kumbukumb u ya vipigo viwili, ikishinda michezo sita na sare mmoja.

Wenyeji wa mchezo huo wakiwa chini ya kocha Cedrick Kaze, inashuka ikiwa katika nafasi ya pili kutokana na ushindi wa Azam juzi dhidi ya Dodoma Jiji na kufikisha pointi 25, mbili mbel;e ya Yanga, wakati Simba ikiwa na 19 katika nafasi ya tatu.

Linapokuja suala la Simba na Yanga, wenyeji watakuwa wenye hasira zaidi kutokana na kipigo kizito cha mchezo wa mwisho walipokutana wakati Wekundu wa Msimbazi wakishinda mabao 4-0 kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA.

Yanga itakuwa na presha zaidi kutokana na kuwa na wachezaji na kocha mpya, ambao wamejinasibu kuwa bora kwa matokeo ya uwanjani licha ya kutopata ushindi mnono.

Ni mtihani wa Kaze

Kaze, ambaye alichukua mikoba ya Zaltko Krmpotic atakuwa na kibarua zaidi kuwaaminisha mashabiki wa Yanga kuwa ni kocha sahihi kuwa na miamba hiyo kwa sasa.

Hii inakuwa mechi ya kwanza ya watani wa jadi kwa Kaze, kwani wakati Yanga inavuna pointi nne kati ya sita za msimu uliopita katika Ligi Kuu ilikuwa chini ya Boniface Mkwassa ‘Master’ aliyekuwa akikaimu nafasi ya kocha mkuu, kabla Luc Eymael aliyeisimamia Yanga ikishinda bao 1-0.

Kwa upande wa Simba, kocha raia wa Ubelgiji, Sven Vandebroeck alikuwepo katika mechi zote tatu za watani zilizopita, akipata sare ya mabao 2-2, akafungwa 1-0 na kisha ushindi wake wa 4-0 katika Kombe la FA.

Vita ya viungo

Usajili wa Yanga wa msimu huu umeongeza pia eneo la kati, wakati Mukoko Tonombe akijihakikishia ufalme kwenye eneo la kiungo mkabaji, akiwa na msaada wa wenyeji kama Feisal Salum ‘Fei Toto’, Haruna Niyonzima, Zawadi Mauya, Abdulaziz Makame ‘Bui’, wakati ujio wa Tuisila Kisinda ukiongeza ushindani kwa Deus Kaseke, Juma Mahadhi na Farid Musa.

Simba inaendeshwa zaidi na fundi kutoka Zambia, Clatous Chama, akiwa na Luis Miquessone, Jonas Mkude, Larry Bwalya, Hassan Dilunga, Said Ndemla na Mzamiru Yassin.

Eneo la katikati linaonekana kuwa bora zaidi hasa kwa Simba, ambao wamekuwa na kawaida ya kupitia katikati.

Yanga inatumia zaidi mawinga wao, ambao wana faida ya kuwa na kasi kwa Farid Musa, Kisinda na mshambuliaji anayetokea pembeni, Ditram Nchimbi.

Ushambuliaji

Hakuna shaka kuwa Simba ndiyo inaongoza zaidi katika upachikaji wa mabao, lakini hilo haliwapi uhakika wa Simba kuibuka na ushindi dhidi ya Yanga.

Takwimu hizo zilianza misimu miwili iliyopita, wakati Meddie Kagere akiwa kinara wa mabao, lakini walishindwa kutamba katika mechi mbili za Ligi Kuu msimu uliopita.

Wakiwa na Michael Sarpong, Waziri Junior na Yacouba Sogne, mabingwa hao wa zamani, Yanga wanaweza kuwa na vurugu zaidi katika lango la Simba, hasa kutokana na kuwa na uwezo mkubwa wa kucheza mipira ya vichwa.

Majeruhi tatizo

Kwa mujibu wa makocha wa timu zote mbili, Chama, Chris Mugalu, Kagere, Niyonzima na Carlos Carlinhos hawatakuwa sehemu ya mchezo huo.

Kocha wa Yanga, Kaze alisema Niyonzima ni mgonjwa wa malaria na wamempa ruhusa kuendelea na kambi ya timu ya taifa ya Rwanda alikoitwa, wakati Carlinhos na Balama Mapinduzi wakiendelea kuwa nje kwa maumivu tofauti.

Kocha wa Simba, Sven alisema Chama aliumia katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar, hivyo hana hali nzuri ya kuanza, wakati Mugalu bado hajapona pamoja na Kagere, huku kiungo wa Ghana, Benard Morrison akitumikia adhabu ya mechi tatu.

Wasemavyo wadau

Kiungo wa zamani wa Yanga, Salum Telela alisema mchezo wa leo utakuwa vita katika eneo la kiungo kutokana na timu zote kuwa na wachezaji bora eneo hilo huku pia vita nyingine ikiwa upande wa washambuliaji wa Simba dhidi ya mabeki wa Yanga.

“Kwenye kiungo itakuwa balaa kwani timu zote zina wachezaji hatari eneo hilo na ndiyo wanaweza kuamua mechi kama timu mojawapo itakuwa bora zaidi eneo hilo.

Pia, Yanga imeonekana ina safu kali ya ulinzi na Simba wapo vizuri kwenye ushambuliuaji, hivyo eneo hilo pia itakuwa ni vita kali,” alisema Telela.

Nyota wa zamani wa Taifa Starss, Mohammed Aolph Rishard alisema mechi ya leo itaamuliwa zaidi na viungo kwani timu zote zina watu wa kazi eneo hilo, hivyo itakuwa mechi ya kibabe.

“Hii mechi ya viungo, ndiyo wataamua matokeo kwamba timu ipi inashinda, kwani ukiangalia timu zote zina viungo wazuri wanaoweza kuchezea mpira na hata kukaba, hivyo itategemea wataamkaje siku hiyo (leo) na watakuwa katika ubora upi, alisema Rishard.

Ushindi kwa Yanga utaihakikishia timu hiyo kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu kwa wiki mbili hadi michezo ya ligi itakaporejea kutokana na kupisha timu za taifa.

Nyota wa Taifa Stars wataingia kambini mara baada ya mchezo huo wa leo kwa ajili ya maandalizi ya kuivaa Tunisia katika mchezo wa kufuzu kwa Afcon.