VIDEO:Mamia wamfariji baba aliyepoteza mke, watoto watatu

VIDEO:Mamia wamfariji baba aliyepoteza mke, watoto watatu

Muktasari:

Mamia ya wananchi wamejitokeza katika ibada ya kuaga miili ya watu watano wa familia moja waliofariki dunia Oktoba 13, 2020 baada ya kukosa hewa kutokana na sehemu ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuteketea kwa moto.

Dar es Salaam. Mamia ya wananchi wamejitokeza katika ibada ya kuaga miili ya watu watano wa familia moja waliofariki dunia Oktoba 13, 2020 baada ya kukosa hewa kutokana na sehemu ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuteketea kwa moto.

Ibada hiyo imefanyika Pugu Stesheni jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa pia na viongozi wa dini, wanasiasa wakiwemo wagombea ubunge wa jimbo la Ukonga kwa tiketi ya CCM, Chadema na ACT-Wazalendo.

Katika ajali hiyo, Edward Katemi aliwapoteza Jackline Frank, ambaye ni mkewe, Esther mwenye miaka 15 (mdogo wake na mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Pugu) pamoja na watoto wake watatu; Edwin (mwanafunzi wa Shule ya Msingi Pugu Station, Edison (Green Hill) na Ivon mwenye umri wa miaka minne.

Katemi kwa sasa amebaki na mtoto mmoja, Erick anayesoma darasa la sita shule ya Green Hill ambaye siku ya tukio alikuwa  amepelekwa shuleni kuanza kulala bwenini, takribani saa nne kabla ya moto kushika nyumba yao iliyopo mtaa wa Pugu Stesheni, ikawa ndiyo nusura yake

Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ofisa Kata ya Pugu Station, Zuberi Ibrahim alisema, “Ni jambo la kusikitisha. Tayari viongozi walifika hapa tangu siku ya kwanza na walishaagiza uchunguzi ufanyike kwa sasa tuiombee familia ya mwenzetu Edward Katemi, ana wakati mgumu, familia ya mama Jacky hali kadhalika na wengine waliofiwa.”

Akiendesha ibada ya kuaga miili hiyo, Mchungaji kiongozi kutoka Kanisa la FPCT, Mchungaji Philipo Mdalaga alisema katika misiba ndipo watu hupata funzo la maisha, hivyo ni muhimu kuishi kwa wema na kuwa karibu na kila mmoja.

Hata hivyo, alisema ni wakati wa kumshukuru Mungu na si kuanza kutafuta visababishi kwani kwa kufanya hivyo ni kumkosea Mungu.