Vigogo Chadema kizimbani wakidaiwa kuwashambulia wasimamizi

Muktasari:

Viongozi watano wa Chadema Wilaya ya Tarime mkoani Mara, akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji Tarime, Khamisi Nyanswi wamepandishwa kizimbani kujibu mashtaka ya kuwashambulia na kuwajeruhi wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wilayani humo.

Mwanza. Viongozi watano wa Chadema Wilaya ya Tarime mkoani Mara, akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji Tarime, Khamisi Nyanswi wamepandishwa kizimbani kujibu mashtaka ya kuwashambulia na kuwajeruhi wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wilayani humo.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, wasimamizi wanaodaiwa kushambulia katika tukio lililotokea mjini Tarime Novemba 5, 2019 ni Alex Matungwa na Simon Nyamhanga.

Wengine waliofikishwa mahakamani katika kesi hiyo ya jinai namba 531/2019 ni Pamba Mwita, Stephen Matiko, Mkapa Nyamhanga na Samuel Orwa.

Washatakiwa wote wamepelekwa mahabusu hadi Jumatatu Novemba 11, 2019 maombi ya dhamana zao yatakaposikilizwa na kuamuliwa.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Alhamisi Novemba 7, 2019  Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe amesema jeshi hilo linaendelea kuwasaka watu wengine ambao hakuwa tayari kuwataja majina wala idadi yao kwa tuhuma za kuhusika kwenye tukio la shambulio dhidi ya wasimamizi wasaidizi hao.

“Watuhumiwa ambao tayari wamefikishwa mahakamani pamoja na wengine ambao bado tunawatafuta wanadaiwa kuwashambulia wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi walipokuwa wakibandika kwenye mbao za matangazo orodha ya majina ya wagombea walioteuliwa na walioenguliwa,” amesema Kamanda Mwaibambe