Vijana ACT- Wazalendo waeleza msimamo uchaguzi Serikali za mitaa

Muktasari:

Ngome ya Vijana ya chama cha ACT- Wazalendo imesema inafanya mawasiliano na jumuiya za vijana za vyama vingine vya upinzani nchini Tanzania ili kuitumia siku ya uchaguzi wa Serikali za mitaa Novemba 24, 2019 kudai haki ya demokrasia nchini.

Dar es Salaam. Ngome ya Vijana ya chama cha ACT- Wazalendo imesema inafanya mawasiliano na jumuiya za vijana za vyama vingine vya upinzani nchini Tanzania ili kuitumia siku ya uchaguzi wa Serikali za mitaa Novemba 24, 2019 kudai haki ya demokrasia nchini.

Imesema fedha zitakazotumika katika uchaguzi huo ambao tayari vyama saba vya upinzani vimejitoa, zinatakiwa kuelekezwa katika shughuli nyingine za maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Novemba 16, 2019 naibu katibu mkuu wa ngome hiyo, Bonifasia Mapunda amesema ikiwa CCM watafanya kampeni za uchaguzi huo zinazoanza kesho, vijana wa chama hicho watafanya kila njia ‘kuwavurugia’.

Mapunda amesema vijana wa chama hicho wapo tayari kwa mapambano na wanachokisubiri ni maelekezo ya viongozi wao wa juu.

Ameliomba Jeshi la Polisi kutozuia shughuli zitakazofanywa na vyama vya upinzani, kuhakikisha wanatoa ulinzi.

“Polisi wasidhani wanaweza kushinda nguvu ya umma, kazi yetu ni kuwapa taarifa na wao kazi yao ni kulinda hivyo acheni vitisho kwani maandamano ni haki ya kikatiba kwa wananchi," amesema.