Vijana waaswa kutumia muda kutafuta maarifa

Muktasari:

Wanafunzi wa Barbro Johansson wapewa mafunzo ya utunzaji fedha na kutakiwa kutambua mchango wao kama vijana kwenye taifa

Dar es Salaam. Kaimu Mkurugenzi wa  Benki ya NMB, Ruth Zaipuna amewataka vijana nchini kutambua nafasi yao katika kujenga uchumi na kutumia muda wao vizuri kwenye mambo yanayofaa.

Zaipuna ameyasema hayo alipokutana na wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana Barbro Johansson Model walipotembelea makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam.

Kaimu Mkurugenzi huyo amewaeleza wanafunzi hao kuwa wataweza kutimiza malengo yao endapo watatumia muda mwingi kutafuta maarifa na si vinginevyo.

“Mnatakiwa kutambua kuwa vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa, kwa nafasi ambayo mnayo sasa ni vyema mkawekeza nguvu na muda wenu kwenye kusoma kwa bidii ili muweze kutimiza malengo,” amesema  Zaipuna.

Katika ziara hiyo wanafunzi hao wamepata nafasi ya kujifunza matumizi sahihi ya fedha ikiwemo kuweka akiba benki pamoja na kujionea shughuli za kibenki zinavyofanyika.

Mmoja wa wanafunzi hao Nicole ameeleza kuwa ziara hiyo imemfungua macho na kumfanya aelewe vitu vingi  kwenye masuala ya fedha na benki tofauti na alivyokuwa hapo awali.