Viongozi CCK wavutana chama hicho kushiriki uchaguzi Serikali za mitaa

Friday November 8 2019Katibu wa CCK, Renatus Muabhi

Katibu wa CCK, Renatus Muabhi 

By Elizabeth Edward na Bakari Kiango, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wakati katibu wa CCK, Renatus Muabhi  akisema chama hicho hakitashiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa, mwenyekiti wake, David Mwaijojele amesema kitashiriki.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo asubuhi Ijumaa Novemba 8, 2019, Muabhi amesema hawashiriki kwa sababu wamegundua washindi katika uchaguzi huo wameshaandaliwa.

Katika mkutano wa vyama 11 vya siasa vilivyotangaza kushiriki uchaguzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam leo, Mwaijojele alilieleza Mwananchi kuwa watashiriki kwa kuwa yeye ndio msemaji wa mwisho wa chama hicho.

Katika maelezo yake, Muabhi amesema hawashiriki kwa kuwa mazingira ya uchaguzi si rafiki kwa vyama vya upinzani.

“Tunajitoa kuonyesha jinsi tunavyoidai demokrasia na haki, hatutaki kuwa sehemu ya wasindikizaji katika uchaguzi ambao tayari washindi wameandaliwa.”

“Wagombea walijaza fomu na kuzipeleka, hawakurudishiwa walipofuata siku inayofuata ofisi zilikuwa zimefungwa yaani tunachokiona ni figisu tumeona tujitoe hatuwezi kushiriki kwenye uchaguzi wenye hila namna hii,” amesema Muabhi

Advertisement

Kwa upande wake Mwaijojele alisema CCK hakitasusia uchaguzi na wamekubaliana na vyama vingine 10 kushiriki kikiwemo TLP, Ada Tadea, ADC na NRA.

 

Mwandishi: Tumesikia mmejitoa kushiriki uchaguzi lakini tunakuona uko hapa na  vyama vingine 10 mkitangaza kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Mwaijojele: Nani kasema, mimi ndio msemaji wa mwisho katika chama.

Mwandishi:  Katibu wako Muabhi ndio kasema.

Mwaijojele:  Anajifurahisha huyo, hatujawahi kukaa hata siku moja kukubaliana na mchakato huu. CCK ni taasisi inaongozwa na katiba na kanuni na mimi ndio msemaji wa mwisho. Nasema tutashiriki na bado tunafuatilia mchakato wa rufaa zetu tuna imani haki itatendeka.

Advertisement