Viongozi chama cha ushirika Kigoma kizimbani kwa wizi, utakatishaji fedha

Muktasari:

Watu watano wakiwemo viongozi watatu wa chama cha ushirika cha Kalinzi Coffee Farmers Group  wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma kwa tuhuma za wizi na utakatishaji fedha zaidi ya Dola 74,000 sawa na zaidi ya Sh115 milioni.

Kigoma. Watu watano wakiwemo viongozi watatu wa chama cha ushirika cha Kalinzi Coffee Farmers Group  wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma kwa tuhuma za wizi na utakatishaji fedha zaidi ya Dola 74,000 sawa na zaidi ya Sh115 milioni.

Wakisomewa mashtaka hayo leo Jumanne Januari 21, 2020 na wakili wa Serikali,  Raymond Kimbe  mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Kitalo Mwakitalu  washtakiwa hao walikana makosa yao.

Washtakiwa hao ni Charles Hume,  Yothani Daniel na  Orest Luziro wanaoshtakiwa kwa makosa manne ya wizi na utakatishaji fedha.

Washtakiwa wengine, Linael Komba na Elianaswe Minja ambao ni wafanyakazi wa kiwanda cha Tanganyika Coffee Curing Co Ltd (TCCCO), wanakabiliwa na kosa la kukisababishia hasara chama cha ushirika cha Kalinzi Oganic Coffee Growers.

Amesema Hume, Daniel na Luziro walifanya makosa hayo katika Benki ya NMB manispaa ya Kigoma ambako waliiba Dola 41,000 za Marekani ambazo ni zaidi ya Sh64 milioni mali ya chama hicho.

"Kosa la pili ni Februari 2, 2012 katika eneo la Benki ya NMB waliiba zaidi ya Dola 33,000 za Marekani ambao ni zaidi ya Sh51 milioni ali ya Kalinzi Oganic Coffee Growers,” amesema wakili Kimbe.

Katika kesi hiyo Hakimu Mwakitalu  amesema mshtakiwa Komba na Minja makosa yao yana dhamana, kwamba mshtakiwa wa kwanza hadi wa tatu makosa yao hayana dhamana.