Viongozi wanne Tanzania kuongoza SADC

Mkuu wa Idara ya Viwanda na ushindani katika Jumuiya hiyo, Dk Johansein Rutaihwa

Muktasari:

Viongozi wanne wa Tanzania watakabidhiwa rungu la kuongoza ngazi mbalimbali za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika(SADC) katika kipindi cha mwaka mmoja utakaokoma Agosti, 2020.

Dar es Salaam.  Viongozi wanne wa Tanzania watakabidhiwa rungu la kuongoza ngazi mbalimbali za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika(SADC) katika kipindi cha mwaka mmoja utakaokoma Agosti, 2020.

Wa kwanza ni mwenyekiti wa taasisi  ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Salum Shamte ambaye Jumatatu Agosti 5, 2019 alikabidhiwa jukumu la kuongoza Baraza la Biashara linalounganisha taasisi za sekta binafsi ndani ya jumuiya hiyo  kwa lengo la kuibua na kujadili fursa na changamoto kisha kuzitafutia ufumbuzi.

Wa pili ni katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Faraj Mnyepe atakayekabidhiwa jukumu la kuwa mwenyekiti wa makatibu wakuu ambao ni maofisa waandamizi wa nchi za SADC kupitia mkutano utakaofanyika Agosti 9 hadi 12, 2019.

Tatu, ni Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi atakayebidhiwa jukumu la kuwa mwenyekiti wa baraza la mawaziri wa Mambo ya Nje katika mtangamano huo kupitia mkutano utakaofanyika wiki ijayo Agosti 13 na 14, 2019.

Nne, ni Rais wa Tanzania John Magufuli atakabidhiwa kijiti cha kuongoza jumuiya hiyo kupitia mkutano mkuu wa 39 wa wakuu wa nchi na Serikali utakaofanyika kati ya Agosti 17 na 18, 2019.

 Rais Magufuli atakuwa mwenyekiti wa SADC kuanzia Agosti 17, 2019 hadi Agosti 17, 2020.

 Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Agosti 7, 2019 mkuu wa Idara ya Viwanda na ushindani katika Jumuiya hiyo, Dk Johansein Rutaihwa amesema Rais Magufuli ameshajipambanua kupitia kauli mbiu ya kuimarisha mazingira wezeshi ya kufanyia biashara na jumuishi ya kukuza sekta ya viwanda.

“Kila kitu atakachokuwa akikifanya (Rais Magufuli)  ni lazima kijibu hiyo kauli mbiu yake kwa hiyo sekta binafsi ya Tanzania itafanya kazi kwa ukaribu sana na serikali kujua matakwa yake  na sekta binafsi ni yapi ndani ya SADC ili kutekeleza kauli mbiu yao.”

“Watakapokuwa wanaondoka madarakani wanatakiwa watueleze ni kipi hasa wamefanikiwa kupitia kauli mbiu hiyo,” amesema.

Wali, msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas amesema hatua hiyo ni heshima kwa Tanzania na msukumo mkubwa wa nchi  itakuwa ni kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili.

“Moja ya ajenda ya mwenyekiti itakuwa ni kusukuma lugha ya Kiswahili , kwanza sisi (Tanzania) ndiyo kitovu cha SADC tumesaidia katika ukombozi, ziko lugha nyingi zinazungumzwa Afrika lakini lugha kubwa ya asili ni Kiswahili,” amesema Dk Abbas.