Viongozi wa dini, wadau wataka mazungumzo uchaguzi wa mitaa

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu Bakwata, Sheikh Khamisi  Mataka

Dar es Salaam. Kutokana na sintofahamu ya uchaguzi wa serikali za mitaa, wadau waliozungumza na Mwananchi wamesema meza ya mazungumzo ya pamoja na kuundwa kwa chombo huru cha kusimamia kazi hiyo ndiyo suluhisho la matatizo.

Uchaguzi wa viongozi hao, ambao ni ngazi ya kwanza ya mfumo wa uongozi wa Serikali, umepangwa kufanyika Novemba 24, lakini tayari vyama sita vikubwa vya upinzani vimejitoa vikipinga uendeshaji wake kwa madai kuwa una upendeleo.

Tayari Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo ameshatoa kauli nne katika muda wa takriban wiki moja, akijaribu kurekebisha, kufafanua na kuelekeza wasimamizi wa uchaguzi, jambo ambalo limekosolewa na wapinzani wakihoji madaraka yake kisheria.

Hadi sasa, CCM imeshapata ushindi wa zaidi ya asilimia 90 kutokana na wagombea wa upinzani kukutwa na kasoro kadhaa, ambazo wamezipinga wakidai ni za kutengeneza.

Chadema, NCCR-Mageuzi, ACT-Wazalendo, CUF, Chauma na UPDP vimeshatangaza kujitoa huku vikishauri kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi kusimamia uchaguzi huo badala ya Tamisemi.

Lakini Waziri Jafo amesema wagombea waliochukua fomu, kurejesha au kukata rufaa ndio watakaoruhusiwa kushiriki hata kama vyama vyao vimejitoa, ikiwa ni tofauti na kauli aliyoitoa siku moja kabla kuwa wagombea wote walioenguliwa warejeshwe.

Hali hiyo imesababisha uchaguzi huo kuwa katika hali ya utata, ikionekana kugawa wananchi.

“Siasa imewekewa nyenzo mbili za kisheria na meza ya mazungumzo kwa hiyo ninachoweza kuwashauri wanasiasa ni kutumia nyenzo hizo,” alisema Shekh Hamisi Mataka, mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) alipoulizwa ushauri wake kuhusu uchaguzi huo.

“Mahakama zipo na baraza lao lipo, lakini tunaona halitumiki. Niwashauri kipindi kama hiki watumie nyenzo walizowekewa.”

Sheikh Mataka alisema suluhisho la haraka kwa sasa ni kuwepo kwa meza huru ya mazungumzo.

Alisema Baraza la Vyama vya Siasa ndilo linalotakiwa kuwakutanisha wanasiasa na wadau wengine kwa ajili ya mazungumzo ili suluhu ipatikane mapema.

Sheikh Mataka alieleza kuwa kwa sababu siasa ni mchezo maalumu unaoongozwa na kanuni, ikiwa baadhi ya vyama vitabaini havijatendewa haki, mahakama inaweza kuwasaidia.

Lakini kulikuwa na mawazo tofauti yasiyopingana kutoka kwa Askofu Benson Bagonza wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

“Kwa uchaguzi huu wa serikali za mitaa kinatakiwa chombo huru kusimamia uchaguzi huu,” alisema Askofu Bagonza.

“Ili uchaguzi mkuu wa 2020 nao uwe wa huru na haki, tunahitaji Tume Huru ya Uchaguzi.

“Tamisemi na wasimamizi wasaidizi hawawezi na wakiweza hawataaminika. Hapa ni suala la imani tu, ikitiwa dosari uchaguzi unaharibika. Kunatakiwa chombo huru na kishirikishe vyama vyote.”

Naye ofisa habari wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), John Kamoyo alishauri kuwepo kwa meza ya mazungumzo ili kuondoa kasoro zinazolalamikiwa kwa sasa.

“Watafikia muafaka wakikaa kwenye meza moja ya mazungumzo,” alisema Kamoyo.

“Naishauri Serikali ikutane na wadau wengine wazungumzie jambo hili ingekuwa nzuri zaidi.”

Alisema uchaguzi mkuu ndilo eneo ambalo wananchi wanapata haki ya kupiga kura na kumchagua kiongozi wanayemtaka, hivyo ni muhimu upatikane muafaka.

Mwingine aliyeshauri kuwepo kwa meza ya mazungumzo ni mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba aliyesema yafanyike mazungumzo ya haraka yatakayowakutanisha wadau na kushauri kuundwa kamati ya siasa itakayosaidia kutoa ushauri kwa Tamisemi wakati wa mchakato huo.

“Tarehe 24 haipo mbali, ni keshokutwa tu. Kwa hiyo lazima wakae mezani wakubaliane ili kwa muda huu mfupi lipatikane suluhisho,” alisema Kibamba.

“Watanzania hawataki chombo kingine chochote kisimamie uchaguzi wa aina yoyote zaidi ya NEC. Tamisemi hawana utaalamu na ujuzi wa kusimamia jambo hili.”

Alisema sintofahamu inayoendelea haipaswi kupuuziwa kwa sababu inasababisha madoa kwenye uchaguzi.

“Watu wanafikiri matukio ya kuchoma ofisi yanajitegemea. Sasa kama huu uchaguzi umeanza kuwa na dalili hizi mbaya, je uchaguzi wa mwakani utakuwaje? Wito wangu ni mazungumzo ya haraka lazima yafanyike,” alisema Kibamba.

Alisema mbali na uchaguzi huo kutosimamishwa na Tamisemi, unapaswa kuhamishiwa kwenye uchaguzi mkuu badala ya kuutenganisha kama ilivyo sasa.

“Kuna nchi wana karatasi tano kuanzia juu mpaka chini, sisi tukiongeza serikali za mtaa kwenye uchaguzi mkuu tutakuwa na karatasi nne tu za kupigia kura, hakuna kinachoshindikana,” alisema Kibamba.

Viongozi wa kisiasa wamekuwa wakishauri kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi ili kuweka ushindani wa kweli katika uchaguzi na pia kuwepo kwa meza ya mashauriano wakati wa matatizo ya kisiasa.

Miongoni mwa kasoro zinazolalamikiwa ni pamoja na wasimamizi wasaidizi kutokuwepo ofisini wakati wagombea wa upinzani wakienda kuchukua fomu au kurejesha, kupewa fomu zisizo sahihi na kuenguliwa isivyo sahihi.