Viongozi watakiwa kutosubiri ziara za ma DC, RC kutatua migogoro

Wednesday January 15 2020

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti akizungumza na wenyeviti wa mitaa, vijiji na vitongoji vya mkoa huo, mjini Babati. Picha na Joseph Lyimo 

By Joseph Lyimo, Mwananchi [email protected]

Babati. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amewataka wenyeviti wa vitongoji na vijiji mkoani humo  kutosubiri ziara za wakuu wa wilaya na mikoa kutatua migogoro na kero zinazowakabili wananchi.

Amesema ndio sababu katika ziara za viongozi hao, wananchi huja na mabango yanayoeleza kero na changamoto zinazowakabili.

Mnyeti alieleza hayo Jumanne Januari 12, 2020 wakati akizungumza na wenyeviti wa vijiji na vitongoji Mkoa wa Manyara.

Amesema kiongozi anayesubiri ziara ili atatue changamoto zinazowakabili wananchi hafai kuwa katika nafasi hiyo.

"Mwenyekiti ndio Rais wa kijiji ukiwa na wajumbe 25 wa kijiji ambao ndio washauri wako na ukashindwa kutatua migogoro ya eneo lako ni wazi umeshindwa kutimiza wajibu wako,” amesema Mnyeti.

Mwenyekiti wa mtaa wa Tanesco wilayani Simanjiro, Justin Abraham amesema wamejengewa uwezo mkubwa wa kutambua wajibu wao tofauti na awali.

Advertisement

"Nadhani mwenye masikio amesikia maagizo na ushauri mbalimbali uliotolewa na mkuu wetu wa Mkoa, sisi  tutakwenda kutekeleza kwa maendeleo ya wananchi wetu," amesema.

Makamu Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Christopher Chengula amesema semina elekezi  zinatakiwa kutolewa kila mara kwa wenyeviti wapya ili kuwajengea uwezo zaidi.

Chengula amesema wenyeviti wengi wa mitaa, vijiji na vitongoji ni wapya na kupitia semina hiyo elekezi watapata mwanga  katika kutimiza wajibu wao.

Advertisement