Visima vya maji ya chumvi hospitali ya Nkinga vyazua balaa

Tuesday November 5 2019

Mkurugenzi mtendaji wa hospitali ya Nkinga,

Mkurugenzi mtendaji wa hospitali ya Nkinga, wilayani Igunga,Victor Ntundwe,akitoa taarifa ya hospitali hiyo kwa Waziri wa Maji,Prof Makame Mbarawa katika kijiji na kata ya Nkinga.picha na Robert Kakwesi. 

By Robert Kakwesi, Mwananchi rkak[email protected]

Tabora. Ukosefu wa maji ya uhakika na matumizi ya maji ya visima yenye chumvi, yamesababisha vifaa katika hospitali ya Rufaa ya Nkinga iliyopo wilayani Igunga, Tabora Tanzania kuharibika.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara leo Jumanne Novemba 5, 2019 katika Kijiji cha Nkinga, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Nkinga, Victor Ntundwe amesema kuna visima viwili chakavu vilivyojengwa mwaka 1984 kwa lengo la kuhudumia watu 550.

Amesema visima hivyo vinatoa maji yenye chumvi ambayo yanaharibu vifaa vya maabara na kliniki ya meno.

Amemweleza Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa kuwa kwa sasa hospitali hiyo ina watu 1,600 huku mahitaji yakiwa ni lita 244,000 na kusababisha pampu za maji kuungua mara kwa mara.

Mkurugenzi huyo, amemuomba Waziri wa Mbarawa kuifikiria hospitali hiyo kupata maji kutoka mradi wa Ziwa Victoria ambayo hayana chumvi hivyo kunusuru  vifaa vya hospitali hiyo.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Igunga, John Mwaipopo, ameungana na Mkurugenzi huyo kutaka sio tu maji hayo yaunganishwe katika Hospitali ya Nkinga, bali na maeneo mengine ya kata hiyo na ya jirani.

Advertisement

Amesema Kata ya Nkinga ni ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya watu ikitanguliwa na Igunga mjini na kwamba, kupelekewa maji ya uhakika kutawasaidia wakazi hao wanaoteseka kupata maji safi na salama.

Akijibu maombi hayo, Waziri Mbarawa, amesema Serikali inawajali wananchi na maombi yao yamekubaliwa na Serikali.

“Ndugu zangu nimetumwa na Rais John Magufuli niwaambie kuwa tutawaletea maji ya Mradi wa Ziwa Victoria hapa kwenu,” amesema.

Profesa Mbarawa amesema mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria umefikia asilimia 83-84 na kwamba, mwishoni mwa mwezi huu, wananchi wa Igunga na Nzega wataanza kunufaika na mradi huo kwa kupata maji.

Amesema Serikali itaanza mpango wa kusambaza bomba kwenda Nkinga kutoka bomba kuu eneo la Ziba umbali wa kilomita 25 na kutengenezwa tenki la juu.

Pia, amesema imeamriwa kujengwa mfumo mzuri wa usambazaji wa maji na wale wenye uwezo kuunganisha kwenye nyumba zao na wasio na uwezo wawekewe magati.

Advertisement