Vita mpya Chadema

Dar es Salaam. Umeya wa Jiji la Dar es Salaam umeiingiza Chadema kwenye vita mpya dhidi ya CCM na Serikali ili kumwokoa meya wao asing’olewe.

Chadema inapambana kuzuia Baraza la Halmashauri ya Jiji hilo kuamua hatma ya Isaya Mwita juu ya kuendelea kuongoza jiji hilo kubwa nchini.

Wakati mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana akiitisha kikao maalumu cha baraza la madiwani kesho, wao Chadema wamekimbilia mahakamani kuweka zuio la mjadala wa meya wake, Mwita wakati wa kikao hicho.

Lengo la kikao hicho cha madiwani ni kupokea taarifa ya uchunguzi dhidi ya tuhuma za Mwita baada ya tume iliyoundwa kuchunguza suala hilo kukamilisha kazi yake.

Barua ya Sipora ambayo Mwananchi imefanikiwa kuiona inaeleza kikao hicho kitakuwa na ajenda ya kufungua kikao, kupokea taarifa ya timu ya uchunguzi dhidi Meya Mwita kwa ajili ya uamuzi na kufunga kikao.

Mwananchi lilimtafuta Mwita kujua kama amepata barua hiyo, alijibu, “Nimepata barua leo (jana) pamoja na wajumbe wengine wa baraza la jiji.”

Mwita kwa mara nyingine aliwaomba viongozi wa dini wamwombee kwa sababu lolote linaweza kutokea.

Meya huyo aking’olewa litakuwa pigo kwa Chadema kwani itajikuta ikipoteza meya wa pili katika mkoa wa Dar es Salaam.

Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Chadema ilipata mameya watatu katika jiji la Dar es Salaam, ambao walikuwa Mwita (Dar es Salaam), Charles Kuyeko (Ilala) na Boniphace Jacob (Kinondoni).

Hata hivyo, Jacob alihamia Ubungo baada ya Kinondoni kugawanywa, ambayo ilitwaliwa na CCM wakati Kuyeko aliamua kuihama Chadema na kujiunga na CCM.

Pia Mwita akiondoka litakuwa pigo jingine kwa Chadema kupoteza uongozi wa jiji baada ya Kalist Lazaro kujivua umeya wa Arusha na kujiunga na CCM hivi karibuni.

Pamoja na kupoteza mameya hao, Chadema pia imepoteza wabunge, madiwani na makada wengi walioamua kujiunga na CCM tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Ikitokea mpango huo wa kumng’oa ukafanikiwa, jiji hilo litaongozwa na Naibu Meya Abdallah Mtinika anayetokana na CCM hadi muda wa baraza hilo utakapomalizika takribani miezi mitatu ijayo.

Uwezekano wa kung’oka ni mkubwa hasa ikizingatiwa kati ya wajumbe 16 wanaounda baraza hilo CCM ni tisa na upinzani saba.

Hata hivyo, changamoto iliyopo kwa Mwita ni kuwa katika hao wapinzani saba mmoja ni CUF, ambaye amekuwa anaunga mkono hoja za CCM.

Katika kamati iliyoundwa chini ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ilianza kufanya kazi ya kuhoji baadhi ya wajumbe wa baraza la jiji hilo tangu mwaka 2019.

Miongoni mwa tuhuma anazokabiliana nazo Mwita ni kutotumia Sh5.8 bilioni za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda). Fedha hizo ni asilimia 51 ya hisa zilizotolewa na kampuni ya Simon Group kama sehemu ya ununuzi wa asilimia 51 ya hisa za Uda.

Tuhuma nyingine ni kutumia vibaya gari ya ofisi ambayo alipata nalo ajali, kushindwa kuongoza kikao cha baraza la madiwani na kusababisha meya wa Ubungo Boniface Jacob kugombana na meya wa Temeke, Abdallah Chaurembo na kudaiwa kuwapendelea baadhi ya mameya kuingia kwenye kamati za fedha.

Hata hivyo, Mwita ambaye pia mjumbe wa kamati kuu ya Chadema, alishajibu tuhuma hizo akisisitiza hahusiki na jambo hilo bali ni za kutengenezwa ili kuondolewa katika kiti hicho alichokitumikia kwa miaka minne.

Chadema yatinga mahakamani

Katika kuhakikisha Mwita anasalia madarakani hadi baraza litakapovunjwa, Chadema wameshafungua kesi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuweka zuio la kudumu la kuzuia mchakato wowote wa kumuondoa.

“Kesho (leo), ndiyo kesi inasikilizwa saa 4.00 asubuhi na tayari barua za wito za kuwaita mahakamani mkurugenzi wa jiji, mkuu wa mkoa na mwanasheria mkuu zimeshatolewa,” alisema Alex Masaba ambaye ni wakili wa Chadema Kanda ya Pwani

Kinachotokea sasa kwa Chadema kwenda kortini ili Mwita asing’olewe kinafanana na kile kilichotokea wakati wa uchaguzi wa mwaka 2016 ambapo CCM walikwenda mahakamani kuweka zuio la kufanyika kwa uchaguzi wa meya.

Uchaguzi huo baada ya kuahirishwa zaidi ya mara mbili kati ya Januari na Februari mwaka 2016, Rais John Magufuli aliingilia kati na kuwataka wana CCM wenzake kukubali matokeo ya kushindwa.

Lazima ang’oke

Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdallah Chaurembo alikaririwa na Mwananchi hivi karibuni akidai kuwa mabaraza ya madiwani yanaongozwa kwa mujibu wa kanuni na kipengele cha maadili ndicho kilichosababisha wakaanzisha mchakato wa kutokuwa na imani na Mwita.

“Dhamira kubwa ya kuwapo kwa halmashauri ni kutatua kero za wananchi. Ni kweli Mwita ameshindwa kusimamia majukumu yake kwa ufanisi ikiwamo kuruhusu kama mameya wote kuingia kwenye kamati ya fedha jambo ambalo ni kinyume.

“Tusiangalie muda wa uongozi uliobaki, leo mtu akiwa mbadhirifu lazima umuondoe. Ukweli ni kwamba kung’oka atang’oka tu kwa sababu anamkwamisha Rais John Magufuli hasa kitendo cha kukataa matumizi ya Sh5 bilioni wakati wananchi wa Dar es Salaam wanahaha kutafuta madarasa,” alisema.

Alichokisema Mbowe

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kinachotokea ni mwendelezo wa vyama vya upinzani kubanwa na kutoheshimiwa kwa misingi ya mfumo wa vyama vingi vya siasa na dhima nzima ya wananchi kuwa na mamlaka.

“Tumeona madiwani, wabunge wakihamishwa kwenye vyama, uonevu kwa viongozi wetu wa upinzani unaendelea kwa hiyo kinachotokea hakuna jipya kwani huu ndio utawala tuliona nao.

“Kinachotokea Dar es Salaam kilitokea Karatu (mkoani Manyara), Siha (Kilimanjaro), Babati (Manyara) na maeneo mengi ambayo mameya na wenyeviti wetu wameondolewa,” alisema Mbowe.