Vita vya Kagera vilivyombakisha Nyerere madarakani

Baada ya Tanu kumpitisha kugombea urais mwaka 1975, Mwalimu Julius Nyerere alionya dhidi ya utamaduni uliokuwa unajengeka wa kumpitisha mtu mmoja kila mara na kutaka chama hicho kiangalie wengine wenye nguvu.

Ilikuwa ni ishara tosha kuwa hakutaka kipindi kingine cha kuongoza nchi, lakini hilo halikuwezekana mwaka 1980 wakati uchaguzi mkuu ulipowadia, ikiwa ni miaka michache baada ya kumalizika kwa vita vya Kagera.

Vita vya Kagera vilidumu kwa miezi sita kuanzia Novemba 1978 hadi Aprili 1979 ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 1980.

Msingi wa vita hiyo ambayo Mwalimu Nyerere aliitangaza Jumamosi ya Novemba mosi, 1978 ni kujibu mashambulizi ya majeshi ya Uganda yaliyovamia Kagera na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.

Baada ya kuongoza kwa mafanikio mapambano hayo yaliyomng’oa Rais Idd Amian Dada wa Uganda, Mwalimu Nyerere aliombwa tena aendelee na urais na jina lake likapitishwa katika mkutano maalum wa CCM uliofanyika Septemba 25, 1980.

Zaidi ya wajumbe 1,600 walipokea na kulikubali pendekezo la kumteua Mwalimu Nyerere kugombea tena kiti hicho lililotolewa na Halmashauri Kuu ya Taifa katika kikao chake cha Septemba 18 na 19, 1980 kilichofanyika mjini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo, kabla ya kuanza kuzungumzwa kwa ajenda hiyo ya uteuzi wa mgombea pekee wa urais, Mwalimu Nyerere alikabidhi kwa muda uenyekiti wa mkutano kwa makamu mwenyekiti wa CCM, Aboud Jumbe na kisha aliondoka ukumbini.

Akiwa mwenyekiti wa muda wa mkutano huo, Jumbe aliwasilisha pendekezo la jina la Mwalimu Nyerere kwa niaba ya Halmashauri Kuu ya Taifa kutokana na kuzingatia mambo aliyoyafanya katika kipindi cha miaka mitano 1975—1980.

Wakati Jumbe alipouliza ni wajumbe wangapi wanaafiki pendekezo hilo, wajumbe wote walikubali na alipotaka kujua wasioafiki, hakuna mjumbe aliyepinga na ndipo Nyerere alipotangazwa rasmi kwamba ameteuliwa kuwa mgombea pekee wa kiti hicho.

Baadaye, Mwalimu Nyerere aliitwa kurejea kwenye ukumbi wa mkutano kujulishwa uamuzi wa mkutano wa kumteua kuwa mgombea pekee wa urais wa Jamhuri ya Muungano katika uchaguzi wa 1980.

Muasisi huyo wa Taifa alikubali ombi la CCM, ambayo ndio kwanza ilikuwa na umri wa miaka mitatu tangu izaliwe mwaka Februari 5, 1977.

“Mwalimu Nyerere alisema huo utakuwa muhula wa mwisho akisema anatengeneza utamaduni wa kuachiana madaraka tangu mwaka 1975,” anasema Dk Azaver Lwaitama, mhadhiri mwandamizi wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Hata hivyo, Dk Lwaitama anasema baada ya vita ya Kagera, ilikuwa vigumu kwake kung’atuka kwa kuwa hali ya uchumi haikuwa nzuri, akimkariri Nyerere akisema “nikitoka hapa nitakuwa natoroka matatizo”.

Dk Lwaitama anasema mwaka 1975 Mwalimu Nyerere aliwahi “kudokeza kwamba angekaa pembeni kidogo na mwingine aingie madarakani”.

Anasema kifo cha rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Aman Karume kilichotokea Aprili 7, 1972 kwa kupigwa risasi akiwa jengo la makao makuu ya Afro-Shirazi (ASP), kuondolewa madarakani kwa Rais wa Uganda, Dk Milton Obote na Idd Amin mwaka 1971 kiliwafanya watu kumshawishi aendelee kubaki.

Dk Lwaitama anasema Mwalimu Nyerere alikubali kugombea mwaka 1975 akisema ungekuwa muhula wake wa mwisho, lakini haikuwezekana kwa kuwa aliendelea hadi 1985 aliposema “kama tatizo la kubaki madarakani ni matatizo, hayo matatizo hayatakwisha kila awamu yatakuwapo”.

Sababu za kukubali kugombea

Katika hotuba ya kuwashukuru wajumbe wa mkutano huo kwa uamuzi wao, Mwalimu Nyerere alisema kulikuwa na sababu mbili zilizomfanya akubali tena kugombea kiti cha Urais.

“Kutokana na hali ya uchumi wa nchi kwa sasa ambayo si nzuri,” alisema Nyerere. “Na, pili, ni haja iliyopo ya kuandaa utaratibu wa mabadiliko ya uongozi wa juu.”

Alisema sababu kubwa ni haja ya kuandaa utaratibu wa mabadiliko ya uongozi ambayo lazima yafanyike kwa faida ya nchi. Kwa upande wa matatizo ya uchumi, Mwalimu Nyerere alisema kwa hali ya wakati ule, ilikuwa wajibu wa kila mmoja kufanya kila aliloweza kulivusha Taifa kutokana na matatizo hayo.

“Kubadili nahodha si jambo baya, lakini kama si lazima kabisa kufanya hivyo, basi si vibaya kusubiri mpaka mawimbi yakatulia kidogo,” alisema Mwalimu.

Alisema “nilipoteuliwa kama hivi mwaka 1975 nilisema kwa kirefu kidogo kabla sijaukubali mzigo huu. Nilisema mambo mawili. Kwanza, nilieleza haja ya kuunganisha Tanu na ASP kuwa chama kimoja”.

“Hilo sasa tumefanya, na matokeo yake ni CCM. Nchi yetu tuliyoiita nchi ya chama kimoja ingawa kwa kweli ilikuwa na vyama viwili sasa ni nchi ya chama kimoja kweli. Nadhani tuna haki ya kujipongeza kwa mafanikio hayo,” alisema.

“Matatizo ya uchumi yako ya aina mbili. Kwanza tunayo yale ya muda mrefu na ambayo yanazikabili nchi zote zinazoendelea. Pili, tunayo haya ya muda mfupi, yaliyotokana na mafuriko, ukame na vita, ambayo ni yetu.

“Ni dhahiri kwamba matatizo tunayoyasema ni haya ya muda mfupi, si yale ya muda mrefu kwa maana tukiyafanya hayo ya muda mrefu kuwa ni sababu ya kutobadili Rais wa Jamhuri, basi tungelazimika kuchagua rais wa maisha.”

Matokeo yatangazwa

Baada ya kushinda uchaguzi, Mwalimu Nyerere alitangazwa kuwa mshindi wa mbio za urais Oktoba 31 na Chifu Adam Sapi Mkwawa, aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi.

Idadi ya wananchi waliopiga kura ilikuwa watu milioni 5.95 na kati ya hao wapigakura milioni 5.5 walimpa Nyerere kura za “Ndiyo”, ikiwa ni sawa na asilimia 93.01 na wengine 259,040 walipiga kura za “Hapana”.’ Kura 157,019 ziliharibika.

“Hivyo basi kwa mujibu wa kifungu cha 6 ibara ya 4(a) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, sasa natangaza rasmi kuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere amechaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Chifu Mkwawa.

Mawaziri washinda

Katika uchaguzi huo mawaziri wengi walishinda, lakini wabunge wengi wa zamani, wakiwamo mawaziri wawili, walishindwa.

Walioshinda ni Abel Mwanga, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Cleopa Msuya (Viwanda), Alphonce Mwingira (Ardhi, Nyumba na Maendeleo Mijini), Amir Jamal (Fedha) na Chediel Mgonja (Utamaduni wa Taifa na Vijana).

Waziri Mkuu, Edward Sokoine, alipita bila kupingwa katika jimbo la Monduli hali kadhalika Jackson Makweta, (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu) naye pia alipita bila kupingwa.

Mawaziri waliopoteza viti vyao walikuwa ni Solomon ole Saibul (Mifugo na Maliasili), na Nazar Nyoni (naibu, Elimu ya Taifa).

Aapishwa, aunda baraza

Mwalimu Nyerere aliapishwa Novemba 5 na Jaji Francis Nyalali na mara baada ya kuapishwa alisema atamchagua Waziri Mkuu mpya badala ya Edward Sokoine ambaye “ameomba kuacha kazi hiyo kutokana na afya yake”.

Siku mbili baadaye, Mwalimu alimteua Cleopa Msuya.

Aliunda baraza lililokuwa na wizara 23, huku mawaziri 10 na naibu waziri mmoja wakiwa wapya.

Baraza jipya lilikuwa na wizara mbili mpya; Wizara ya Madini na Wizara ya Mifugo. Kutokana na mabadiliko hayo shughuli za utamaduni ziliunganishwa na mambo ya habari na kuunda wizara moja inayoitwa Wizara ya Habari na Utamaduni.

Shughuli za maliasili ziliunganishwa tena na utalii na kuunda Wizara ya Maliasili na Utalii. Kutokana na kuundwa kwa wizara mpya ya madini, wizara ya zamani ya maji, nguvu na madini ilibadilika na kuwa Wizara ya Maji na Nishati.

Pia waliteuliwa mawaziri watatu wasiokuwa na wizara maalumu, mawaziri wawili wa nchi katika ofisi ya Rais na mawaziri wawili wa nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais na mawaziri wawili wa nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu.

Baraza la Mawaziri liliwajumuisha Makamu wa Rais, Aboud Jumbe Mwinyi; Cleopa Msuya (Waziri Mkuu); Amir Jamal (Fedha), Salim Ahmed Salim (Mambo ya Nje), Abdallah Twalipo (Ulinzi), Joseph Mungai (Kilimo), Ibrahim Kaduma (Biashara), Muhidin Kimario (Mambo ya Ndani).

Wengine ni Basil Mramba (Viwanda), Benjamin Mkapa (Habari na Utamaduni), Aaron Chiduo (Afya), Thabitha Siwale (Elimu), Julie Manning (Sheria), Alnoor Kassum (Maji na Nishati), na John Malecela aliyekuwa Waziri wa Madini.

Pia Herman Kirigini aliteuliwa kuwa Waziri wa Mifugo, Isaac Sepetu (Maliasili na Utalii), Samuel Sitta (Ujenzi), Augustine Mwingira (Mawasiliano na Uchukuzi), Alfred Tandau (Kazi na Ustawi wa Jamii), Mustafa Nyang’anyi (Ardhi,a Nyumba na Maendeleo Mijini), wakati mawaziri ambao hawakuwa na wizara maalum walikuwa ni Rashidi Kawawa, Abdallah Natepe na Daniel Machemba.

Mawaziri wa Nchi katika ofisi ya Rais walikuwa ni Timothy Shindika na Clement George Kahama, wakati Kigoma Malima na Aboud Talib Aboud waliteuliwa kuwa katika ofisi ya Makamu wa Rais (Mipango na Uchumi).

Mawaziri wa nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu walikuwa ni Jackson Makweta (Mambo ya Mikoa) na Abdiel Mwanga (Maendeleo ya Utumishi).

Walioteuliwa kuwa manaibu waziri ni Venance Ngula (Fedha), Seif Bakari na Stephen Kibona (Ulinzi), Ali Mchumo (Mambo ya Ndani) na Chrisant Mzindakaya (Viwanda).

Baraza la Mawaziri lilikutana kwa mara ya kwanza Jumatatu ya Novemba 10, 1980 tangu ulipomalizika uchaguzi mkuu wa mwaka huo.