Vita ya rushwa, Takukuru yatoa ombi kwa viongozi wa dini na wazazi

Muktasari:

  • Kongamano maalum juu ya nafasi ya vyuo vya elimu ya juu katika mapambano dhidi ya rushwa limefanyika leo Ijumaa Desemba 13, 2019 Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) nchini Tanzania ambapo viongozi wa dini na wazazi wameombwa kutokwepa jukumu la kuwafunzisha waumini na watoto madhara ya rushwa.

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nchini Tanzania imewaomba viongozi wa dini na wazazi nchini humo kutumia nafasi zao kutoa mafunzo ya athari ya rushwa katika jamii.

Hayo yalisemwa leo Ijumaa Desemba 13, 2019 na Kibeshi Kiyabo kwa niaba ya mkurugenzi mkuu wa Takukuru wakati akiwasilisha mada ya ‘uadilifu ni silaha katika vita dhidi ya rushwa’ lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Amesema rushwa ina madhara makubwa kwa jamii na taifa kwa ujumla inapaswa kukemewa kuanzia ngazi ya familia, kanisani, misikitini na maeneo ya shule na vyuo.

"Viongozi wa dini wanapaswa kutumia kama agenda suala hili la rushwa, ihubiriwe makanisani na misikitini ili waumini waweze kufahamu madhara yake na wao waikemee katika mazingira wanayoishi," amesema Kiyabo

Ameendelea kusema, "Turudi katika malezi yetu. Wazazi turudi katika misingi yetu ya kuwafundisha watoto maadili mema kuanzia ngazi ya familia ili watoto hawa wanapokwenda shule na hatimaye kufikia chuo kikuu wajue ubaya wa rushwa."

Kiyabo amesema taasisi za elimu ya juu zina jukumu kubwa la kufundisha maadili kwa wanafunzi.

"Rushwa iwe kubwa au ndogo ina madhara na rushwa ni vita yetu sote. Lazima tuikemee kwani madhara yake ni makubwa zaidi na hatupaswi kuifumbia macho," amesema Kiyabo

Amidi wa Shule Kuu ya Sheria ya UDSM, Profesa Hamudi Majanga akiwasilisha mada ya 'Mchango wa elimu na mitalaa katika mapambano dhidi ya rushwa' amesema Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa na ili kutekelezwa, suala la rushwa linapaswa kufundishwa ngazi ya elimu ya juu.

Naye Sospeter Makubi akiwasilisha mada ya kodi na rushwa kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) amesema nchi zenye rushwa zinapoteza asilimia nne ya mapato yake (GDP) na hii inatokea hasa katika nchi zinazoendelea.

Amesema vichocheo vikubwa vya rushwa ni wale wasiopenda kulipa kodi kwa njia zinazostahili hivyo kutengeneza mianya ya rushwa na kwa baadhi ya watumishi wa TRA kutokuwa na maadili ya kazi yao na wengine kutaka kupata mafanikio ya haraka.

Makubi ametaja maeneo yenye viashiria vya rushwa ni eneo la uingizaji wa mashine za kielektroniki za (EFD), ukaguzi wa kodi na uondoaji wa mizigo ya forodha na magari.

Amesema Mitaala ya elimu ya juu ijumuishe suala la maadili ili kuwafundisha wanafunzi madhara ya rushwa na kudumisha ushirikiano ili kutokomeza rushwa na kuongeza makusanyo ya kodi.